In Summary

•Mpenzi wa marehemu aliwapeleka polisi kwenye duka alilonunua gunia ambalo aliuweka mwili wa mwanamke huyo .

•Mshukiwa alifahamisha maafisa kuwa walikuwa na ugomvi wa kinyumbani na alimpiga marehemu kichwani na kumuua papo hapo.

Mwili wa mwanamke ulipatikana ukiwa umefungwa kwenye sanduku huko Ruiru
Image: HISANI

Mpenzi wa mwanamke ambaye mwili wake ulipatikana ukiwa umewekwa kwenye sanduku na kutupwa nje ya nyumba ya makazi katika mtaa wa Kamakis,  eneo la Ruiru, Kaunti ya Kiambu alikamatwa kuhusiana na mauaji hayo.

Polisi walisema mwanamume huyo alikiri mauaji ya mwanamke huyo aliyetambuliwa kama Rispa Ndunge Vaati, 27, kutoka Kaunti Ndogo ya Kitui Kusini.

Mpenzi wa marehemu aliwapeleka polisi kwenye duka alilonunua gunia ambalo aliuweka mwili wa mwanamke huyo kabla ya kuuacha takriban mita 500 kutoka walipokaa.

 

Tukio hilo la mauaji lilitokea Jumatatu, Aprili 17.

Alisema aliuingiza mwili huo kwenye begi na baadaye kwenye gunia kabla ya kuuacha katika eneo la tukio.

Mshukiwa huyo pia alifahamisha maafisa kuwa yeye na mpenziwe walikuwa wakifanya kazi katika hoteli moja eneo la Kamakis ambapo marehemu alikuwa keshia na mshukiwa alikuwa mpishi.

Alifahamisha maafisa kuwa walikuwa na ugomvi wa kinyumbani na alimpiga marehemu kichwani na kumuua papo hapo.

Kisha mshukiwa aliuweka mwili wa marehemu kwenye sanduku lililokuwa ndani ya nyumba hiyo.

Mshukiwa huyo pia aliwaongoza maafisa hao hadi eneo la Mukuyu, kaunti ya Muranga ambapo pia walipata simu ya marehemu kutoka kwa binamu yake.

Mshukiwa aliambia polisi aligombana na mpenziwe kabla ya kumpiga kwa hasira na akaanguka sakafuni kabla ya kuzimia.

Alipogundua kuwa alikuwa amefariki, aliamua kutafuta njia za kuutupa mwili huo.

Kisha akachukua simu yake ya rununu na kuipeleka nyumbani kwake Murang'a na kuiacha hapo.

Simu hiyo ya rununu ilipatikana Ijumaa asubuhi kama sehemu ya ushahidi.

Mkuu wa DCI katika eneo la Ruiru, Justus Ombati alitaja matukio hayo kama mafanikio katika uchunguzi wa mauaji.

Alisema tukio hilo lilitokea kutokana na ugomvi wa kinyumbani na hasira.

Mwili wa Rispa uligunduliwa na wenyeji ambao waligundua sanduku limewekwa kwenye mlango wa makazi.

Sanduku hilo lilikuwa limewekwa kwenye gunia wakati mwili huo ulipopatikana Jumanne alasiri.

Polisi walisema waliitwa kwenye eneo la tukio na kufahamishwa kuhusu ugunduzi huo kabla ya kuupeleka katika chumba cha kuhifadhia maiti.

Mwanamke huyo alikuwa na jeraha kichwani na alikuwa nusu uchi.

Mwili huo uliingizwa kwenye sanduku kabisa na kuachwa mahali ambapo iligunduliwa.

View Comments