In Summary

•Polisi wanachunguza mauaji ya mwanamke mwenye umri wa miaka 24 ambaye sehemu za mwili wake zilipatikana zikiwa zimewekwa  kwenye mfuko wa karatasi

•Kwingineko, wapelelezi wanachunguza kifo cha mwanamke ambaye hajajulikana, ambaye mwili wake ulipatika ukiwa uchi katika mto unaopita Kasarani

Polisi wakiwa nje ya jengo la ghorofa kando ya TRM Drive, Barabara ya Thika mnamo Januari 14, 2023
Image: HISANI

Polisi wanachunguza mauaji ya mwanamke mwenye umri wa miaka 24 ambaye sehemu za mwili wake zilipatikana siku ya Jumapili zikiwa zimewekwa  kwenye mfuko wa karatasi kwenye barabara ya Thika, Nairobi.

Mwanamke huyo alidungwa kisu na kukatwakatwa hadi kufa katika nyumba iliyo karibu na TRM Drive, barabara ya Thika.

Polisi walisema bado hawajajua nia ya mauaji hayo. 

Inaripotiwa kuwa wauaji walijaza baadhi ya sehemu za mwili kwenye mfuko wa karatasi.

Maafisa wa polisi kutoka Kasarani walifika katika eneo la tukio wakauchukua mwili wa marehemu na kuupeleka hadi katika chumba cha kuhifadhia maiti kwa uchunguzi wa maiti. Hatua hii itabainisha uchunguzi wa mauaji hayo.

Kwingineko, maafisa wa upelelezi wanachunguza kifo cha mwanamke ambaye hajajulikana, ambaye mwili wake ulipatika ukiwa uchi katika mto unaopita Kasarani, Nairobi.

Mwili huo ulipatikana Jumamosi, Januari 13.

Kwa mujibu wa polisi, mwili wa mwanamke huyo ulipatikana ukiwa umewekwa ndani ya gunia huku mikono na miguu yake ikiwa imefungwa.

Kufikia sasa, utambulisho wauaji na nia ya uhalifu huo bado haijulikani.

Polisi waliripoti kuwa mwanamke huyo, ambaye mwili wake ulipatikana mtoni katika mtaa wa Lucky Summer, alikuwa na majeraha ya kisu shingoni, ambayo yanaashiria marehemu huenda alijeruhiwa kabla ya kutupwa majini.

Awali ukiaminika kuwa mizigo iliyotupwa, gunia hilo lililochukuliwa na polisi baadaye lilipatikana kuwa na maiti ya mwanamke huyo.

Mwili wake umehamishiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha City, ukisubiri kutambuliwa na kufanyiwa uchunguzi wa baada ya maiti.

Mkuu wa Polisi wa Nairobi, Adamson Bungei, alibainisha kuwa hakuna mtu aliyekamatwa na utambulisho wa mwanamke huyo bado haujajulikana.

Aliongeza kuwa alama za vidole vyake zilikusanywa ili kusaidia katika mchakato wa utambuzi.

Polisi wametoa wito kwa wakenya walio na taarifa zozote kuhusu tukio hilo wajiwasilishe katika kituo cha polisi cha eneo hilo.

"Familia zilizokosa jamaa zao pia zilishauriwa kuzuru chumba cha kuhifadhi maiti cha City ili kusaidia kutambua mwathiriwa," alisema Bungei.

Polisi wanashuku kuwa mwanamke huyo aliuawa kwingine na kutupwa majini kabla ya kusombwa na maji.

View Comments