In Summary

•Bobi Wine alibainisha kuwa Muhoozi na baba yake Rais Yoweri Museveni wamefanya maisha nchini Uganda kuwa magumu.

•Bobi Wine alisema matamshi ya Muhoozi kuwa ni ya kipuuzi huku akimtaja kama mnyama anayenyanyasa watu.

Bobi Wine anasema kwamba anawakilisha vijana
Image: EPA

Kiongozi wa chama cha Uganda National Unity Platform (NUP) Robert Kyagulanyi Ssentamu almaarufu Bobi Wine ameungana na Wakenya kumkashifu kamanda wa jeshi wa Uganda Muhoozi Kainerugaba kufuatia matamshi yake ya Jumatatu kuhusu utekaji wa jiji kuu la Kenya, Nairobi.

Katika taarifa yake, Bobi Wine alibainisha kuwa Muhoozi ambaye ni msimamizi wa majeshi ya nchi kavu wa Uganda na baba yake Rais Yoweri Museveni wamefanya maisha nchini Uganda kuwa magumu.

"Wapendwa Wakenya, sasa mnaelewa maana ya kuishi Uganda chini ya Jenerali Museveni na mwanawe, ambaye alipatia cheo cha juu zaidi cha kijeshi na kumweka kuwa msimamizi wa majeshi yetu ya nchi kavu!" alisema kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Bobi Wine alisema matamshi ya Muhoozi kuwa ni ya kipuuzi huku akimtaja kama mnyama anayenyanyasa watu.

"Cha kusikitisha ni kwamba, chini ya machapisho hayo yasiyo na maana kuna mnyama mkubwa ambaye huwatendea unyama na kuwatesa watu wetu kwa ajili ya kujifurahisha!" mbunge huyo wa zamani alisema.

Muhoozi ambaye ana umri wa miaka 49 anatumikia kama kamanda wa majeshi ya nchi kavu ya Uganda People Defence Forces (UPDF).

Aliteuliwa na baba yake katika nafasi hiyo mnamo Juni 2021.

Ilikuwa ni mara ya pili kwa Museveni kumpandisha cheo mwanawe, katika uongozi wa jeshi katika kipindi cha miezi sita.

Katika msururu wa jumbe zake kwenye Twitter, Muhoozi alimtaja aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta kama “kakake mkubwa’ na kumlaumu kwa kukosa kuwania urais kwa muhula wa tatu, na kuongeza kuwa angeshinda uchaguzi kwa urahisi.

"Tatizo langu pekee na kaka yangu mkubwa ni kwamba hakugombea muhula wa tatu. Tungeshinda kirahisi," aliandika.

Mwanawe Museveni alizidi kuidhalilisha Katiba ya Kenya akisema Uhuru alipaswa kubadilisha katiba ili kusalia madarakani.

"Haha! Nawapenda jamaa zangu wa Kenya. Katiba? Utawala wa sheria? Lazima uwe unatania! Kwetu (Uganda), kuna Mapinduzi tu na muda si mrefu mtayafahamu!" alisema.

Kulingana na sheria za Kenya, mara tu Mkuu wa nchi akihudumu kwa mihula miwili, hawezi kugombea muhula wa tatu.

Muhoozi aliendelea kuadai kwamba itamchukua yeye na jeshi lake chini ya wiki mbili kuchukua udhibiti wa Nairobi, mji mkuu wa Kenya.

"Haingetuchukua sisi, jeshi langu na mimi, wiki 2 kuteka Nairobi," alisema.

View Comments