In Summary

•Ruto alisema alifanya mkutano wa faragha na kiongozi huyo wa Wiper na akaomba awe sehemu ya serikali yake lakini akakataa.

•Rais alisema uamuzi wa Kalonzo kukataa ofa yake hautamzuia kutafuta kuungwa mkono na jamii ya Wakamba.

Rais William Ruto na Kalonzo Musyoka kwenye picha ya maktaba.
Image: MAKTABA

Rais William Ruto amefichua kuwa aliwasiliana na Kalonzo Musyoka punde tu baada ya kutangazwa mshindi lakini kiongozi huyo wa Wiper akakataa kuungana naye serikalini.

Ruto alisema alifanya mkutano wa faragha na kiongozi huyo wa kisiasa wa Ukambani na akaomba awe sehemu ya serikali yake lakini akakataa.

“Nilimtafuta, tukakaa akaniambia anataka kubaki Upinzani. Nifanye nini?” alihoji.

Ruto alizungumza wakati wa maombi ya madhehebu mbalimbali katika Kaunti ya Machakos siku ya Jumapili.

“Alikataa, lakini niliamua kwamba hata akikataa, lazima nitafute viongozi wengine wa Kamba wawe serikalini kwa sababu tuna mawaziri watatu na wabunge watatu kutoka eneo la Ukambani. Tutaongeza zaidi,” Ruto alisema.

Rais alisema uamuzi wa Kalonzo kukataa ofa yake hautamzuia kutafuta kuungwa mkono na jamii ya Wakamba na kuwaweka katika nyadhifa kuu.

“Nimekuwa na urafiki wa muda mrefu na jamii ya Wakamba. Nilijiambia sitaendesha serikali ambayo haina jamii hii ndani yake,” alisema.

Walioteuliwa na rais kutoka eneo hilo ni pamoja na aliyekuwa Gavana wa Machakos Alfred Mutua ambaye anasimamia hati ya Masuala ya Kigeni na Diaspora.

Ruto pia alimchagua Peninah Malonza kuongoza sekta ya Utalii.

Eneo hilo pia lina idadi ya wateule wengine wa serikali, akiwemo Jonathan Mueke, Katibu Mkuu, Wizara ya Michezo na Monica Juma, Mshauri wa Rais.

Rais alisema angetamani viongozi kutoka Ukambani wasipeleke jamii mitaani kuandamana dhidi ya serikali.

Aliwataka viongozi wa makanisa kutoka kwa jamii kumwombea Kalonzo akisema yeye ni muungwana lakini yuko upande mbaya wa siasa.

Ruto alisema viongozi wa Upinzani wanapaswa pia kupigania manufaa ya wananchi na wala sio maslahi yao ya kibinafsi.

"Tunapopigania maslahi yetu kama viongozi, tusiharibu maisha ya watu," aliongeza.

Naibu Rais Rigathi Gachagua alihimiza jamii hiyo kukumbatia serikali ya Kenya Kwanza.

Alisema jumuiya hiyo ilikuwa waziri mmoja wakati wa muhula wa mwisho wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta ilhali Ukambani ilimuunga mkono Azimio.

“Mlikuwa watu wa handshake lakini mlikuwa na nafasi moja tu ya waziri. Ikiwa Kalonzo angejiunga nasi, angekuwa amepata kitu,” aliongeza.

Alisema jamii imepata heshima kwa kutokuwa sehemu ya maandamano ya hivi karibuni dhidi ya serikali.

View Comments