In Summary

•Mazishi ya Miles yaliyojaa hisia yalifanyika Jumamosi ambapo wanafamilia, marafiki, majirani na Wakenya wengine walijumuika pamoja kumuaga.

•Kufuatia mazishi yake, baadhi ya Wakenya sasa wamezamia kwenye mitandao ya kijamii kusihi Safaricom kutimiza ombi hilo.

Marehemu Danny Miles alizikwa siku ya Jumamosi, Aprili 8, 2023.
Image: HISANI

Danny Miles, mgonjwa wa saratani aliyeandika ujumbe wa kihisia kwa Safaricom mapema mwaka huu akiiomba kampuni hiyo kumsaidia bintiye wakati akifariki hatimaye alizikwa nyumbani kwao katika eneo la Gem, Kaunti ya Siaya.

Miles ambaye kwa jina halisi  ni Maurice Ocieng alifariki mnamo Machi 21 baada ya kupambana na saratani kwa takriban miaka mitatu..

Mazishi yake yaliyojaa hisia yalifanyika Jumamosi ambapo wanafamilia, marafiki, majirani na Wakenya wengine walijumuika pamoja kumuaga. Alizikwa kwenye jeneza jeupe katika shamba la wazazi wake.

Hata baada ya kuzikwa kwa Miles, Wakenya kwenye mitandao ya kijamii wameendelea kuwasihi Safaricom kutimiza maombi yake na kumsaidia mjane wake Florence  Akoth Odege na binti yao mdogo Britney Ochieng'.

Mwezi Januari, Miles, kupitia mtandao wa Facebook alifahamisha kampuni hiyo  kuwa alihisi kama mwisho wake unakaribia na akaeleza wasiwasi kuhusu hatima ya bintiye mdogo ambaye alikuwa anakaribia kuingia shule.

Alisema kuwa ugonjwa ulitumia pesa zote alizokuwa ameweka kwa ajili ya familia na kumuacha kutegemea msaada wa marafiki.

"Habari Safaricom, mimi ni Maurice Ochieng anayejulikana kama Danny Miles. Ninatoka mjini Muhoron. Mwezi Machi mwaka jana, niligunduliwa na saratani, sarcoma ya tishu laini. Inanitafuna hakika.

Siku kwa siku ninahisi. Nilikuwa nikiweka akiba ili nipeleke familia yangu ndogo kwa likizo lakini nimeishiwa na nguvu, siwezi. Ninaishi kwa msaada wa marafiki. Binti yangu mdogo bado ni mchanga. Bado hajaanza shule. Nilikuwa nafanya mpango lakini nasikitika nimeshindwa kama baba. Mkono wangu wa kushoto ulikuwa umekatwa lakini bado saratani ilizidi kuniathiri

Ninawaomba msaidie binti yangu mara tu nitakapoondoka kwa sababu ninaweza kuhisi. Nambari yangu ni 0706345827. Namba ya mke wangu ni 0757084605 (Florence Odege) au labda mtupeleke safari ya mara moja maishani nitashukuru sana,"  Danny Miles alindikia kampuni ya Safaricom mnamo Januari 19.

Kufuatia mazishi yake, baadhi ya Wakenya sasa wamezamia kwenye mitandao ya kijamii kusihi Safaricom kutimiza ombi hilo.

Mtumizi mmoja wa Facebook aliyehudhuria mazishi aliandika ujumbe mrefu akiwataja wote ambao mjane wa Miles alitambua kwa  mchango mkubwa wakati wa ugonjwa, kifo na mazishi. Alibainisha kuwa kampuni hiyo haikutajwa.

"Danny aliacha watoto wawili. Msichana na mvulana. Timiza matakwa yakwe. Aliwaona kama mwokozi na akawafikia. Alikuja katika muda wake wa haja. Wasimamizi wa ukurasa wa Safaricom wanapaswa kuarifu viongozi ili waweze kutimiza matakwa ya Danny," ujumbe huo ambao umesambazwa sana ulisoma.

Suleiman Shilaku aliandika, "Safaricom huyu ni Danny Miles ambaye aliwasihi kumsaidia kumsomesha bintiye pindi tu atakapoaga. Tafadhali timiza matakwa yake ya mwisho. Mwambieni Mkurugenzi Mtendaji kuwa na huruma kwa mara moja,"

Mandele C. Sungura aliandikia kampuni hiyo, "Mpendwa Safaricom PLC. Nimekuwa mteja wenu shupavu tangu 2009 nilipopata Simcard hii. Danny Miles alizikwa jana na alikuwa na ombi moja tu kwenu! Kuelimisha watoto wake wakati yeye atakapokwenda. Ninaandika haya kukuomba kuwaelimisha watoto hawa chini ya Wakfu wa MPESA. Hii itakuwa Zawadi kamili ya Pasaka kwa familia!

View Comments