In Summary

•Uhuru aliwashukuru wote ambao wamemkumbuka katika siku yake maalum, na pia akawaombea waishi miaka mingi na wawe na afya njema.

•"Acha kuuliza kuhusu miaka, tuseme miaka yoyote ambayo Mungu ametupa, tunamshukuru. Acha kuniuliza maswali mengi kuhusu miaka," Uhuru alisema.

Aliyekuwa rais, Uhuru Kenyatta
Image: MAKTABA

Siku ya Alhamisi, Rais mstaafu Uhuru Kenyatta alivunja ukimya huku Wakenya kutoka kila pembe ya nchi wakimsherehekea mnamo siku yake ya kuzaliwa.

Uhuru anatimiza umri wa miaka 62 leo, Oktoba 26. Rais huyo wa zamani ambaye alishiriki mazungumzo ya dhati na kituo kimoja cha redio cha humu nchini alisema anashukuru kutimiza mwaka mmoja zaidi.

Aliwashukuru wote ambao wamemkumbuka katika siku yake maalum, na pia akawaombea waishi miaka mingi na wawe na afya njema.

"Nashukuru, nashukuru mmenikumbuka, Mungu pia awabariki kwa jinsi mlivyoniombea. Nawaombea muishi miaka mingi na muwe na afya njema. Hata wasikilizaji wenu wote nawaombea sawa. Sina la kusema," mkuu huyo wa nchi wa zamani alisema.

Mtangazaji alikuwa amempigia simu Rais huyo wa zamani moja kwa moja hewani kumtakia heri ya siku ya kuzaliwa.

Waliendelea kutupiana maneno ya mzaha kidogo ambapo Uhuru alitupilia mbali maswali kuhusu umri wake kutoka kwa mtangazaji. Wawili hao walifurahia nyakati za kicheko katikati ya mazungumzo.

"Umetimiza miaka mingapi?" mtangazaji aliuliza.

Uhuru alisema "Acha kuuliza kuhusu miaka, tuseme miaka yoyote ambayo Mungu ametupa, tunamshukuru. Acha kuniuliza maswali mengi kuhusu miaka.”

Aliongeza, “Maisha yanaanzia katika miaka 40, nakuhakikishia hilo kwa sababu umri huo ulipita zamani sana. Na pale ambapo Mungu ametufikisha tunasema asante kwake. Tunaomba muendelee kutuweka katika amani, afya njema. Pia tunaiombea nchi yetu kwa sababu pia inakaribia kutimiza miaka 60,"

Viongozi kutoka pande zote za kisiasa wamemsherehekea na kummwagia sifa Rais huyo wa zamani anapofikisha umri wa miaka 62.

Viongozi hao katika jumbe zao walizungumzia sana uhusiano ambao wamekuwa nao na Uhuru, licha ya wakati mwingine kuunga mkono pande tofauti za kisiasa.

Wafanyibiashara wa Gatundu pamoja na Wakenya kutoka maeneo mengine ya nchi waliandaa sherehe za kumheshimu Rais wa Nne.

Katika sherehe zote, keki zenye picha na majina ya Uhuru zilikatwa.

View Comments