Tammy Abraham kila siku anawatesa mabeki kule nchini Uingereza na barani Ulaya. “Ana uwezo kama Didier Drogba. Anakisaidia kikosi katika safu ya Ulinzi pamoja na kutupia wavuni magoli jinsi anavyojiskia,” Jose Mourinho.

Abraham amekuwa nguzo kuu kwenye kikosi chake Frank Lampard, Chelsea pale ugani Stamford Bridge. Lakini je, wamjua huyu Tammy Abraham ni nani?

KUZALIWA

Tammy Oghenetega Tamaraebi Abraham alizaliwaa mnamo tarehe 2 mwezi October mwaka 1997 mjini London. Babake, Bw. Tamaraebi Bakumo na Bi. Makumo wanatokea taifa la Nigeria.

Wazazi wake Tammy walihamia nchini Uingereza kabla ya mchana nyavu huyu kuzaliwa kwa ajili ya kutafta riziki bora. Tammy Abraham ndiye kifungua mimba wa familia ya watoto 2. Nduguye mdogo anajulikana kama Timmy.

MAISHA YA KISOKA

Tammy Abraham alianzia maisha yake ya soka katika klabu ya Chelsea kwa vijana wasiozidi umri wa miaka minane. “Siku yangu ya kwanza katika klabu ya Chelsea nilipatana na mshambulizi Didier Drogba aliyenipa lift kwa gari lake. Hata hivyo, sikuwa na mfahamu vyema,” Tammy Abraham.

Abraham Alitia sahihi yake ya kwanza mnamo mwaka wa 2014 na klabu ya Chelsea kabla ya kutolewa kwa mkopo msimu uliofuata na kuichezea Bristol City.

Siku Njema huonekana alfajiri. Nyota yake Abraham ilianza kung’aa katika mechi yake ya kwanza na klabu ya Bristol kwani alifunga goli la kwanza kwenye ushindi wao wa 2-1 dhidi ya Wigan. Abraham alirejea klabuni Chelsea alikokisaidia kikosi cha vijana wasiozidi umri wa miaka 19 kutwaa taji la klabu bingwa barani Ulaya.

Msimu wa 2017/2018 Abraham alijiunga na kikosi cha Swansea City baada ya mkufunzi wa Chelsea wakati huo, Antonio Conte kumtema katika kikosi cha kwanza. Tammy Abraham alifunga goli lake la kwanza kwenye Ligi kuu nchini uingereza kwenye ushindi wa 2-0 dhidi ya Crystal Palace.

Msimu huo ulikamilika huku Tammy Abraham akiwa na magoli 8 kutoka mechi 38.

Msimu wa 2018/2019 dua lake Tammy Abraham lilirejea baada ya kujiunga na Aston Villa katika Championship. Tammy alicheka na wavu mara 26 katika mechi 40. Jambo hili lilimfanya Mkufunzi mpya wa klabu ya Chelsea, Frank Lampard kumpa nafasi katika kikosi chake cha kwanza.

Msimu wa 2019/2020 umekua wa aina yake katika maisha yake Tammy Abraham. Abraham amecheka na wavu mara tisa kwenye Ligi kuu nchini Uingereza. Frank Lampard amefichua kuwa Tammy ndiye mshambulizi nambari moja kwenye kikosi chake.

Baada ya kuwa na uwezo wa kuyachagua mataifa mawili kwenye kitengo cha timu ya taifa, Tammy Abraham ameamua kujiunga na Uingereza.

Juhudi za timu ya taifa ya Nigeria kumshawishi akubali ,”SUPER EAGLES,” ziliambulia patupu.

-Albanus Kiswili.

View Comments