haaland

Bwenyenye wa Chelsea Roman Abramovich bado ana imani watamsajli kinda wa Norway Erling Haaland mwishoni mwa msimu huu.  Nyota  huyo wa Borussia Dortmund mwenye umri wa miaka 20  alisaidia klabu yake kufuzu kwa robo fainali ya kombe la klabu bingwa bara ulaya, baada ya kufunga magoli mawili.  

Halaand alijiunga na Dortmund kutoka Salzburg, na  Abramovich yuko tayari kutoa zaidi ya pauni million 100 ili kumpata. 

Hizi ni baadhi za habari za soka ulimwenguni;

Kiungo wa Everton Abdoulaye Doucoure atakaa nje kwa muda wa wiki kumi kutokana na jeraha la mguu.  Mfaransa huyo mwenye umri wa miaka 28, alikosa mechi ya ligi dhidi ya Chelsea Jumatatu,  na madaktari wamethibitisha amevunjika mfupa wa mguu. Doucoure amecheza mechi 25 tangu kujiunga na Toffees kutoka Watford msimu huu. Kocha wake Carlo Ancelotti anatumai atarejea kabla ya msimu kukamilika.

Manchester United imetangaza kuwa bwenyenye Avram Glazer anauza hisa zake za pauni millioni tano. Iwapo atauza kama inavyotarajiwa, Glazer atapata pauni millioni 71.5 huku United ikikosa kupata chochote kutokana na biashara hio. Vile vile familia ya Glazier ambao ni wanahisa wakubwa wa klabu hio watashuka kutoka asilimia 78 hadi 74.9 kufikia Jumanne ijayo.

Polisi wanaendelea na uchunguzi baada ya watu wawili wasiojulikana kuingia katika uwanja wa Fulham, na pia simu za rununu kutumika kupeana habari za ndani za klabu hio. Wawili hao ambao walivalia suti nyeusi, wanaaminika kufanya ujasusi na huenda walikua na nia ya kufanya mashambulizi ya kigaidi.

Shirikisho la soka nchini Uingereza pia limevitaka vilabu vyote kuweka mikakati kambambe ya usalama ili kuzuia watu wenye nia mbaya kudhuru wanamichezo.

Meneja wa AFC Leopards Tom Juma anasema bado ni mapema sana kudai kuwa watanyakua taji la ligi kuu nchini msimu huu, licha ya kuwa katika hali dhabiti. Ingwe wameanza vyema msimu huu na wanashikilia nafasi ya tatu kwenye jedwali baada ya mechi 13 na wanapigiwa upato kunyakua taji hilo kwa mara ya kwanza tangu mwaka wa 1998. 

Juma anadai licha ya kuwa wana kikosi kizuri bado timu kadhaa zina uwezo wa kushinda ligi ya  FKF hivyo lazima wajikakamue zaidi, ili kusalia kileleni.

View Comments