In Summary

• "Nimeratibu mbio sita za Diamond League, mashindano mawili ya World Athletics Continental Tour na mawili ya Kenya," Omanyala alisema.

Bingwa wa Jumuiya ya Madola katika mbio za mita 100 Ferdinand Omanyala baada ya kuweka rekodi mpya ya mita 60 mjini Lievin Picha: HISANI

Mshikilizi wa rekodi ya Afrika na bingwa wa mbio za mita 100 wa Jumuiya ya Madola Ferdinand Omanyala ameapa kunyakuwa taji la kimataifa katika Riadha za Dunia za 2023 mjini Budapest baadaye mwaka huu.

Mashindano hayo ya kimataifa yameratibiwa kufanyika Agosti 19 hadi 27 na mwanariadha huyo raia wa Kenya anaamini kuwa ana uwezo kutamba katika ulingo huo. Omanyala alizungumza siku moja baada ya kuweka rekodi mpya ya kitaifa ya mita 60 huku akimshinda bingwa wa Olimpiki wa mita 100 Marcell Lamont Jacobs nchini Ufaransa. Ulikuwa ushindi wa kwanza wa Omanyala dhidi ya Muitaliano huyo.

Afisa huyo wa Polisi alisema ufanisi wake nchini Ufaransa, ambako alishinda mara tatu na kushika nafasi ya pili katika mara moja, ulichochea hamu yake kuwania ubingwa wa dunia.

“Kenya itakuwa bingwa wa dunia mjini Budapest mwaka huu. Nina furaha sana. Nimefurahi sana jinsi nilivyofanya vizuri huko Ufaransa. Inaonyesha tu jinsi msimu utakuwa,” Omanyala alisema. "Nilikuwa na lengo la 6.55 katika ziara yangu mwaka huu, ambayo nilifanikisha kabla ya kuondoka na 6.54 (0.02 haraka kuliko Jacobs)."

Arthur Cisse wa Ivory Coast alimaliza wa tatu kwa sekunde 6.59. Mnamo Februari 3, Omanyala alimaliza wa pili katika mashindano ya Elite Indoor Track Miramas kwa sekunde 6.60 katika ufunguzi wake. Mnamo Februari 8, alishinda mbio za Mondeville katika rekodi ya kitaifa ya sekunde 6.55. Kisha, mnamo Februari 11, alishinda de Paris kwa sekunde 6.56.

Omanyala alifichua ratiba iliyosheheni, ambayo anasema iko katika maandalizi ya Budapest.

"Nimeratibu mbio sita za Diamond League, mashindano mawili ya World Athletics Continental Tour na mawili ya Kenya," Omanyala alisema.

"Kwa sasa ninajiandaa kwa mashindano ya AK, yaliyoratibiwa kufanyika Februari 24 na 25 katika Uwanja wa Nyayo na Machi 10 na 11 katika Uwanja wa Ruring'u huko Nyeri."

Mashindano ya World Athletics Continental Gold Tour nchini Botswana mnamo Aprili 29 na ASA Grand Prix nchini Afrika Kusini Aprili 12 na 19 pia yamo katika orodha yake. Kabla ya Kip Keino Classic jijini Nairobi mnamo Mei 13, atajaribu bahati yake katika Ligi ya Almasi ya Doha mnamo Mei 5 kabla ya kwenda Rabat Mei 28, Monaco mnamo Julai 21 na Roma Juni 2.

Mnamo Septemba 8, atashiriki Ligi ya Almasi ya Brussels akiwa na matumaini ya kufuzu kwa fainali za Prefontaine Classic, zilizopangwa kufanyika Septemba 16-17.

View Comments