Bingwa wa Kenya na Afrika katika mbio za mita 100 Ferdinand Omurwa Omanyala amesema haelewi kabisa kilichotokea katika fainali za mita 100 kwenye Mashindano ya Dunia jijini Budapest, Hungary ambapo alishindwa.
Omanyala ambaye alikuwa amejikakamua sana kufuzu kwa fainali hizo aliibuka wa 7 katika mbio hizo ambazo zilishindwa na mwanariadha wa Marekani Noah Lyles. Alichukua sekunde 10.07 kukamilisha.
Wakati akizungumza baada ya mbio hizo, mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 27 alidokeza kuwa mwili wake ulishindwa kufanya vizuri wakati wa mbio hizo.
"Leo mwili haukuwa ukifanya kazi, sijui nini kilitokea lakini nitaenda kuketi na kuona kilichotokea," Omanyala alisema.
Alisema atachukua muda wake, kukaa chini na kutazama tena mbio hizo ili kufahamu ni nini hasa kilifanyika akapoteza.
“Championships huwa na mambo yake, mambo yanatokea kwenye michuano hiyo. Ndivyo ilivyo. Lazima nirudi nyuma, nione na kushughulikia kila kitu kilichotokea na kuangalia ni masuluhisho gani tunayohitaji kuwa nayo,” alisema.
Omanyala alisema ndoto yake ya kushinda Mashindano ya Dunia inaendelea kubaki hai hadi itimie. Alipoulizwa kuhusu mbio zake zijazo, alisema atahitaji kuketi na wasimamizi wake kabla ya kuamua hatua yake nyingine.
"Sijaamua mbio zinazofuata kwa sababu lengo langu lilikuwa kwenye hafla hii," alisema.
Hata hivyo, alisema macho yake yataelekezwa kwenye Michezo ya Olimpiki na mbio zingine kati yake. Pia alikataa kuzungumzia shindano hilo, akisema huwa haangazii sana wapinzani wake.