In Summary

•Faith kipyegon amevunja rekodi yake katika mbio za mita 1500 za wanawake katika mbio za 'Diamond league'  mjini Paris.

•Kipyegon alimaliza kwa saa 3:49.04, na kuipita rekodi yake ya 3:49.11, ambayo iliwekwa nchini Italia mwaka jana.

Faith Kipyegon
Image: Facebook

Mwanariadha wa Kenya Faith Kipyegon  alivunja rekodi yake ya dunia katika mbio za mita 1,500 za wanawake katika  mashindano ya 'Diamond League' mjini Paris mnamo Julai 7,2024.

Kipyegon alimaliza kwa dakika 3:49.04, na kuipita rekodi yake ya 3:49.11, ambayo iliwekwa nchini Italia mwaka jana.

"Nilijua rekodi ya dunia iliwezekana kwa sababu hivi majuzi nilikimbia kwa kasi sana nchini Kenya," alisema Kipyegon, ambaye alitumia  dakika 3:53.98 katika majaribio ya Olimpiki ya Kenya.

Aliongeza ; "Nilikuwa nakuja hapa kukimbia mbio zangu tu na kuona ni namna gani niko katika kutetea taji langu kwenye Olimpiki."

Kipyegon mwenye umri wa miaka 30 ameshinda medali ya dhahabu ya Olimpiki mara mbili katika mbio za 1,500, baada ya kushinda mjini Rio de Janeiro mwaka wa 2016 na Tokyo 2021.

Kabla ya Jumapili, alikuwa amekimbia mara mbili pekee mwaka wa 2024, katika 1,500 na 5,000, hadi kupata nafasi yake kwa michezo ya Olimpiki ya Paris katika majaribio ya Kenya mnamo Juni.

Katika michezo ya Olimpiki ya Paris, tukio kubwa zaidi duniani mwaka huu, Kipyegon ataongeza ubabe wake katika mbio za mita 1500 na 5,000 kama alivyofanya kwenye mashindano ya dunia ya Budapest mwaka jana. .

Katika majaribio ya kitaifa, na kabla ya kuanza maandalizi yake kwa ligi ya Diamond ya Paris ya leo, Kipyegon aliahidi kujikakamua ili kupata ushindi.

Michezo ya Olimpiki itaanza Julai 26 hadi Agosti 11.

View Comments