In Summary

•Kipyegon atashiriki muda uliosalia wa Olimpiki akiwa na onyo kufuatia drama iliyotokea kati yake na Gudaf Tsegay wa Ethiopia.

•Shirika hilo liliweka wazi kuwa nafasi ya medali ya fedha ya bingwa huyo wa mbio za mita 1500 katika mbio za mita 5000 imerejeshwa.

Faith Kipyegon alidaiwa Gudaf Tsegay.
Image: HISANI

Mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za mita 1500 kwa wanawake, Faith Kipyegon atashiriki muda uliosalia wa Michezo ya Olimpiki ya Paris akiwa na onyo kufuatia drama iliyotokea kati yake na Gudaf Tsegay wa Ethiopia wakati wa fainali za mbio za mita 5000 mnamo Jumatatu usiku.

Katika uamuzi uliotolewa usiku wa kuamkia Jumanne, waamuzi wa shirika la riadha duniani waliamua kwamba Kipyegon apewe ushindi wake wa fedha baada ya ushahidi uliowasilishwa dhidi yake kutotosha yeye kuenguliwa katika mbio hizo.

Bingwa huyo wa riadha mwenye umri wa miaka 30 hata hivyo alipewa kadi ya njano ambayo atakuwa nayo kwa muda uliosalia wa Olimpiki ya Paris.

"Waamuzi wa Rufaa wamepitia ushahidi wote uliopo na kukubaliana kulikuwa na mgusano mkubwa kati, na kwa wanariadha hao wawili," Shirika la Riadha Duniani lilisema.

Waliongeza, "Majaji walihitimisha kuwa tukio hilo halikuruhusu kuondolewa katika mashindano. Baraza la Majaji linapenda kueleza wazi kwamba matukio ya aina hii hayakubaliki kamwe na kwa hivyo inapendekeza kwamba Faith Kipyegon apokee kadi ya njano ya kinidhamu ambayo inaweza kudumu katika muda wote uliosalia wa Michezo."

Shirika hilo liliweka wazi kuwa nafasi ya medali ya fedha ya bingwa huyo wa mbio za mita 1500 katika mbio za mita 5000 imerejeshwa.

Jumatatu usiku, rufaa iliyofaulu iliyofanywa na timu inayowakilisha Kenya katika Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024 ilirudisha afueni kwa Kipyegon na mamilioni ya mashabiki wanaofuatilia mashindano ya kimataifa yanayoendelea nchini Ufaransa.

Kipyegon alimaliza katika nafasi ya pili katika mbio za mita 5000 lakini akaondolewa katika mashindano kwa madai ya kumsukuma Gudaf Tsegay wa Ethiopia. Hii ilivunja sio tu moyo wa mwanariadha huyo, bali pia ya mamilioni ya mashabiki ambao walikuwa wakimtazama kote ulimwenguni.

Hatua hiyo ya kusikitisha hata hivyo haikumaanisha mwisho kwani maafisa wa timu ya Kenya walikata rufaa ili uamuzi wa kumuondoa Kipyegon kwenye mashindano utupiliwe mbali, na kwa bahati nzuri, rufaa ilifanikiwa.

"Rufaa iliyofanikiwa ilifanywa na #TeamKenya. Medali ya Fedha ya Faith wa ajabu ilirejeshwa," Timu ya Kenya ilisema katika taarifa usiku wa kuamkia Jumanne.

"Atakuwa amesimama karibu na Beatrice tunapoimba Wimbo wa Taifa kesho. Fedha ya mita 5000 ni ya Faith Kipyegon,” waliongeza.

Bingwa wa rekodi ya dunia ya mbio za mita 10,000, Beatrice Chebet alishinda medali ya kwanza ya dhahabu ya Kenya katika Michezo ya Olimpiki ya Paris katika mbio za mita 5,000 kwa wanawake baada ya kuibuka na ushindi wa dakika 14:28.56 Jumatatu usiku katika uwanja wa Stade de France.

Mshikilizi wa rekodi ya dunia katika mbio za mita 1,500, Faith Kipyegon aliibuka wa pili kwa dakika 14:29.60 lakini mwanzoni alikuwa amepokonywa ushindi baada ya kudaiwa kumsukuma Gudaf Tsegay wa Ethiopia.

Sifan Hassan wa Uholanzi aliibuka wa tatu baada ya kumaliza kwa muda wa dakika 14:30.61 na kutwaa shaba. Nadia Battocletti wa Italia (14:31.64) alishika nafasi ya nne Mkenya mwingine katika mbio hizo Margaret Chelimo aliwekwa wa tano (14:31.64).

View Comments