In Summary

•“Ushuru wa 20% kwa kampuni za kamari utaondoa udhamini kwa vilabu vya kandanda nchini   vilabu hivyo viliandika.

• Wenyekiti Ambrose Rachier na Dan Shikanda wa Gor na AFC mtawalia  wametoa ombi kwa serikali kuondoa pendekezo hilo huku wakisema kuwa kandanda nchini Kenya imekuwa ikidhaminiwa sana na mashirika ya kamari kutoka mwaka wa 2016.

Mashemeji Derby
Image: Hisani

Vilabu vikuu viwili vya kandanda nchini Kenya ambavyo vina ufuasi mkubwa zaidi nchini, Gor Mahia na AFC Leopards vimekosoa ushuru wa bidhaa wa 20% uliotangazwa na waziri wa fedha Ukur Yattani siku ya Alhamisi.

Kupitia barua ya pamoja iliotolewa siku ya Alhamisi, wenyekiti wa vilabu hivyo Dan Shikanda (AFC Leopard) na Ambrose Rachier (Gor Mahia) walitoa ombi kwa serikali kuondoa ushuru huo huku wakisema kuwa hatua hiyo itafurusha wadhamini wa vilabu vingi nchini huku wengi wa wadhamini yakiwa kampuni za kamari.

Ushuru wa bidhaa wa 20% kwa mashirika ya kamari utaondoa udhamini kwa vilabu vya kandanda kwa ligi zote nchini na kusambaratisha shughuli za michezo”  vilabu hivyo viliandika.

Kupitia barua hiyo vilabu hivyo vilieleza kuwa vilabu vya kandanda nchini vimekuwa vikikabiliwa na changamoto nyingi za kifedha na ushuru huo utawafanya wadhamini kushindwa kabisa kuwapa ufadhili.

Litakuwa bao la kujifunga kwa kandanda nchini Kenya kwa kuwa itadhalilisha au hata kukatiza kipindi cha pili cha msimu huu wa kandanda. Hii itakuwa na athari kubwa kwa msimu unaosubiriwa sana wa 2022 ambao unatarajiwa kuwa mwanzo mpya wa mchezo wa kandanda iliyoimarishwa nchini” walisema Shikanda na Racheir.

Hii sio mara ya kwanza kwa serikali kuweka ushuru huo kwani sheria hiyo ilikuwa imetolewa tena mwaka wa 2019. Hata hivyo, sheria hiyo ilifutiliwa mbali kufuatia malalamiko ya umma na mashirika ya kamari.

Rachier na Shikanda wametoa ombi kwa serikali kuondoa sheria hiyo tena huku wakisema kuwa kandanda nchini Kenya imekuwa ikidhaminiwa sana na mashirika ya kamari kutoka mwaka wa 2016.

Kwa sasa Gor Mahia na AFC Leopards wanadhaminiwa na kampuni ya Betsafe.

Akisoma bajeti katika bunge la kitaifa, waziri Ukur Yattani pia alisema kuwa Shilingi bilioni 15 zimetengewa kwa wizara ya michezo nchini.

(Mhariri: Davis Ojiambo)

View Comments