In Summary

•Mechi tisa za kufana zilichezwa wikendi ambayo imetamatika mchuano wa kwanza ukiwa kati ya Crystal Palace na Tottenham Hotspurs ambao ulichezwa mida ya saa nane unusu siku ya Jumamosi.

•Mashabiki wengi kote duniani walitazamia kumuona nyota Christiano Ronaldo akishiriki mechi yake ya kwanza na United baada ya kurejea EPL msimu huu. 

Image: TWITTER

Jedwali la EPL limeanza kuchukua sura huku mashindano hayo yakiingia wiki ya nne.

Mechi tisa za kufana zilichezwa wikendi ambayo imetamatika mchuano wa kwanza ukiwa kati ya Crystal Palace na Tottenham Hotspurs ambao ulichezwa mida ya saa nane unusu siku ya Jumamosi.

Tottenham ilipoteza nafasi yake kileleni baada ya kupokea kichapo cha 3-0 kutoka kwa vijana wa Patrick Viera ugani Selhurst Park.

Mechi sita zilichezwa mida ya saa kumi na moja Jumamosi huku mechi iliyoangaziwa zaidi ikiwa kati ya Manchester United na  Newcastle United.

Mashabiki wengi kote duniani walitazamia kumuona nyota Christiano Ronaldo akishiriki mechi yake ya kwanza na United baada ya kurejea EPL msimu huu. Kama ilivyotarajiwa staa huyo mwenye miaka 36 aling'aa huku akifunga mabao mawili kati ya manne ambayo United waliilaza Newcastle.

Mabao mengine mawili ya United yalifungwa na kiungo matata Bruno Fernandes na Mshambulizi Jesse Lingard huku bao la pekee la Newcastle likifungwa na Javier Manquillo.

Arsenal ilipanda nafasi nne kutoka mkia baada ya bao la mshambulizi Pierre Emerick Aubameyang katika dakika ya 66 kuwapa ushindi wa 1-0 dhidi ya Norwich City ambao kwa sasa wameshikilia nafasi ya mwisho bila pointi yoyote.

Mechi kati ya Southampton na Westham United iliishia sare ya 0-0 huku mabingwa wa ligi kuu msimu uliopita Manchester City wakipata ushindi wa moja kwa sufuri dhidi ya wenyeji Leicester City.

Brentford walipoteza 0-1 dhidi ya wageni wao Brighton huku Wolves wakilaza Watford mabao 2-0 ugenini.

Mechi ya mwisho siku ya Jumamosi ilikuwa kati ya Chelsea na Aston Villa ambapo mabao mawili ya mshambulizi Romelu Lukaku na moja la Matteo Kovacic yalisaidia miamba hao wa London kupata ushindi wa 3-0.

Mchuano mmoja pekee ulichezwa siku ya Jumapili ambapo Leeds United walikaribisha Liverpool ugani Elland Road mida ya saa kumi na mbili unusu jioni.

Hata hivyo Leeds walipokea kichapo cha mabao matatu bila jawabu kutoka kwa wageni wao.

Wiki ya nne ya EPL itakamilika kwa mchuano kati ya Everton na Burnley ambao utachezwa mida ya saa nne usiku wa Jumatatu.

Kwa sasa Manchester United inashikilia nafasi ya kwanza kutokana na wingi wa mabao wakiwa wamepata alama sawa na Chelsea na Liverpool ambao wameshikilia nafasi za pili na tatu mtawalia.

Norwich inashikilia nafasi ya mwisho ikiwa bado haijaandikisha pointi yoyote huku Burnley na Newcastle wakiwa katika nafasi ya 18 na 19 mtawalia na pointi moja kila mmoja.

View Comments