In Summary

•Mulee amesema kwamba alishiriki mkutano pamoja na Shirikisho la soka nchini na akaomba  kuacha nafasi yake kama kocha mkuu wa timu ya taifa mwenyewe.

•Mulee ambaye alitangazwa kama kocha mkuu wa Harambee Stars kwa mara ya 12 mnamo Oktoba 22 mwaka uliopita amesema kwamba tangu atue nchini kutoka India ambako ndugu yake alikuwa anapokea matibabu mwezi Mei mwakani amekuwa akipitia wakati mgumu. 

kocha ghost mulee
Image: the-star.co.ke

Mtangazaji Jacob 'Ghost' Mulee amesisitiza kwamba kuondoka kwake Harambee Stars yalikuwa maafikiano ya pamoja kwa sababu za kibinafsi wala sio kupigwa kalamu kama ilivyoripotiwa kwingine.

Mulee amesema kwamba alishiriki mkutano pamoja na Shirikisho la soka nchini na akaomba  kuacha nafasi yake kama kocha mkuu wa timu ya taifa mwenyewe.

Akizungumza katika kipindi cha 'Gidi na Ghost asubuhi'  siku ya Alhamisi, Ghost alisema kwamba walikuwa na makubaliano mazuri kwenye mkutano huo ambao ulijiri baada ya Harambee Stars kushiriki mechi mbili za kufuzu kucheza kombe la dunia mapema mwezi huu.

"Baada ya kutoka sare mara mbili dhidi ya Uganda na Rwanda, tulikaa chini sote na tukazungumza bila wasiwasi wowote tukakubaliana na shirikisho kwamba ni heri mimi sasa niachie mtu mwingine aweze kusimamia. Nilikuwa na mipango yangu lakini nikasema kwamba si huenda sifanyi kazi nzuri kwa Kenya ilhali niko na mambo yangu ya kibinafsi. Sitakuwa napatia 100% kwa Harambee Stars na tukaelewana na rais wa Shirkisho Nick Mwendwa pamoja na Mkurugenzi Mtendaji. Tulikuwa na makubaliano mazuri sana" Ghost alisema.

Mulee ambaye alitangazwa kama kocha mkuu wa Harambee Stars kwa mara ya 12 mnamo Oktoba 22 mwaka uliopita amesema kwamba tangu atue nchini kutoka India ambako ndugu yake alikuwa anapokea matibabu mwezi Mei mwakani amekuwa akipitia wakati mgumu.

Ghost amesema kwamba ingawa alikabiliwa na masuala yake ya kibinafsi, alifanya jitihada za kuendelea kutoa huduma zake kwa timu ya taifa kwani haingekuwa vyema kujiuzulu kabla ya mechi za kufuzu kombe la dunia kung'oa nanga.

"Nimekuwa nikipitia wakati mgumu sana kwa sababu nilikuwa India kwa kipindi cha miezi miwili na ndugu yangu ambaye alikuwa anaumwa. Kabla ya safari yangu tulikuwa tumecheza  na Misri na Togo lakini baada ya kurejea mambo mengi yalibadilika kibinafsi. Niliangalia nikaona kwamba tunaanza mechi za kuhitimu kombe la dunia na katika ile hali inakuwa vigumu kama kocha kujiuzulu kabla hujaanza kibarua chako" Ghost amesema.

Ameshukuru sana shirikisho la soka kwa kumpa nafasi ya kusimamia timu ya taifa kwa kipindi ambacho amehudumu.

View Comments