In Summary

•Mashabiki wengi wa Newcastle wamekaribisha umiliki huu mpya, wakitumaini uwekezaji huo utaibadilisha timu yao na kufanya vizuri uwanjani, lakini ununuzi huo umekuwa ukishutumiwa kutokana na rekodi za masuala ya ukandamizaji wa haki za binadamu kwenye nchi hiyo ya ghuba ya ufalme wa kiarabu

Image: GETTY IMAGES

Klabu ya ligi kuu ya England Newcastle United imenunuliwa na mfuko mkuu wa umma wa Saudi Arabia, "Public Investment Fund (PIF) kwa thamani ya £300m.

Mashabiki wengi wa Newcastle wamekaribisha umiliki huu mpya, wakitumaini uwekezaji huo utaibadilisha timu yao na kufanya vizuri uwanjani, lakini ununuzi huo umekuwa ukishutumiwa kutokana na rekodi za masuala ya ukandamizaji wa haki za binadamu kwenye nchi hiyo ya ghuba ya ufalme wa kiarabu.

Hizi ni sababu zinazothibitisha utata wa ununuzi huo.

1.Mauaji mabaya ya mwandishi wa habari aliyepinga

Nafasi ya Saudi Arabia kimataifa iliathiriwa kutokana na kifo cha mwandishi Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari wa Saudi aliyekuwa anafanyia shughuli zake Marekani, kilichotokea Oktoba 2018, ambaye alikuwa mkosoaji mkubwa wa serikal ya Saudia.

Mtaalamu mmoja kutoka Umoja wa Mataaifa alisema Khashoggi aliuawa kikatili na timu maalumu kutoka Saudi katika ubalozi wa Saudi huko Uturuki. Mamlaka za Saudi Arabia, akiwemo mwanamfalme Mohammed bin Salman, inayohusishwa na kifo hicho, imekana kuhusika kwao, hata hivyo hadhi yake kimataifa imeharibiwa vibaya na tukio hilo

Mfuko wa Uwekezaji wa Umma wa Ufalme, ambao una hisa 80% huko Newcastle, unasimamiwa na Mwanamfalme Mohammed bin Salman, ingawa Ligi Kuu ilisema imepokea hakikisho kwamba serikali ya Saudi haitahusika moja kwa moja kwenye shughuli za klabu.

2.Kuwatia ndani wanaharakati wa haki za binadamu wanawake

Loujain al-Hathloul aliachiliwa mnamo Februari baada ya karibu miaka mitatu ya kuwa kizuizinI
Image: AFP

Mwaka 2018, Mamlaka za Saudi ziliwakamatwa wanaharakati wa haki za binadamu wanawake 13 waliokuwa wakiongoza kampeni ya kutaka kuondolewa kwa marufuku ya wanawake kuendesha magari. Angalau wananne kati ya wanawake hao 13 walidaiwa kuteswa na kunyanyaswa kingono na wahojiwa.

Mwaka 2020, Mahakama ya ugaidi ilimpata mwanaharakati mashuhuri, Loujain al-Hathloul, na hatia ya uhalifu dhidi ya serikali. Alikanusha mashtaka hayo na wataalam wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa walielezea kuwa yalikuwa mashtaka "ya uwongo".

3.Kukandamizwa kwa wasomi mashuhuri, makasisi na wanamageuzi

Areej al-Sadhan alisema kaka yake Abdul Rahman aliteswa kabla ya kufungwa jela kwa miaka 20 kwa kuandika 'tweets' za kimapenzi ambazo zilikosoa mamlaka
Image: AREEJ AL-SADHAN

Wanaharakati wa haki za wanawake sio watu pekee wanaoshikiliwa kama sehemu ya ukandamizaji dhidi ya wakosoaji nchini Saudi Arabia, ambapo vyama vya siasa, vyama vya wafanyakazi na vikundi huru vya haki za binadamu vimepigwa marufuku.

Watetezi wengi wa haki za binadamu, wasomi, maulamaa na wanamageuzi pia wamekamatwa tangu 2017, kwa sababu tu ya kutumia haki yao ya uhuru wa kujieleza, kulingana na mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu.

Wengi wamekabiliwa na kile Amnesty International imesema ni mashitaka ya uwongo ya ugaidi na makosa ya uhalifu wa kimtandao, na walipewa adhabu kali, ikiwa ni pamoja na adhabu ya kifo.

Siku chache kabla ya kununuliwa kwa klabu ya Newcastle, Mahakama iliidhinisha kifungo cha miaka 20 gerezani alichopewa mfanyakazi wa huduma za kibinadamu mwenye asili ya Saudia na Marekani Abdul Rahman al-Sadhan kwa kukosoa serikali kupitia mtandao wake wa twitter.

4. Vita vikali huko Yemen

Vita nchini Yemen vimesababisha kile Umoja wa Mataifa unasema ni mzozo mbaya zaidi wa kibinadamu kuwahi kutokea duniani
Image: EPA

Saudi Arabia imekosolewa vikali kwa kampeni ya kijeshi katika nchi jirani ya Yemen ambayo imesababisha maafa ya kibinadamu.

Muungano unaoongozwa na Saudi Arabia uliingilia kati mnamo 2015 baada ya waasi wa Yemen kuchukua udhibiti wa sehemu kubwa ya magharibi mwa nchi na kumlazimisha rais kukimbilia nje ya nchi.

Zaidi ya watu 100,000 wameripotiwa kuuawa katika mapigano hayo, huku wafuatiliaji wakieleza kuwepo kwa vifo vya raia 8,700 vilivyotokana na mapigano ya anga.

Makumi ya maelfu pia wanakadiriwa kufa kutokana na sababu zisizo za moja kwa moja, kama ukosefu wa chakula, huduma za afya na miundombinu, wakati kizuizi kidogo cha mzozo huo kimezuia juhudi za kusaidia watu milioni 20 wanaohitaji misaada ya kibinadamu.

Wataalam wa UN wanasema pande zote mbili katika mzozo huo zinaweza kuwa zilifanya uhalifu wa kivita, ingawa muungano huo umesisitiza kuwa unatii sheria za vita.

5.Matumizi makubwa ya adhabu ya kifo

Saudi Arabia inaripotiwa kutekeleza idadi kubw aya adhabu za vifo katika nusu ya kwanza ya 2021 kuliko ilivyofanya katika mwaka mzima wa 2020
Image: ANADOLU AGENCY

Saudi Arabia ni miongoni mwa nchi zinazoongoza duniani katika kutekeleza adhabu ya kifo.

Kwa uchache watu 40 waliuawa kati ya Januari na Julai 2021, kulingana na Amnesty International.

Mnamo Juni, mtu mmoja aliuawa kwa uhalifu ambao anadaiwa kuufanya akiwa na umri wa miaka 17, licha ya hakikisho la hapo awali wa ufalme kwamba ilikuwa imefuta adhabu ya kifo kwa wahalifu wa watoto.

6. Adhabu kwa watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja

Ingawa Saudi Arabia haina sheria kuhusu masuala ya kijinsia au utambulisho wa kijinsia lakini uhusiano wa kimapenzi nje ya ndoa, pamoja na mapenzi ya jinsia moja, ni marufuku kabisa.

Chini ya tafsiri ya nchi hiyo ya sheria ya Kiislamu, adhabu ya kifo ni adhabu inayowezekana kwa wapenzi wa jinsia moja.

Ni kosa kisheria mwanamume kujifanya mwanamke au kuvaa nguo za kike, au kinyuma chake.

View Comments