In Summary

•Masaibu yaliendelea kuandama Mashetani Wekundu katika ziara yao  ya Vicarage Road ambapo Watford iliwaadhibu kwa mabao 4-1 na kuongeza shinikizo kwa kocha Ole Gunnar  Solskjaer ambaye alipigwa kalamu siku ya Jumapili kufuatia msururu wa matokeo mabaya.

•Kwa sasa The Blues wanaendelea kuongoza jedwali na alama 29, City inafuata na 26, Liverpool ya tatu na alama 25, West Ham ya nne na 23 huku wanabunduki wakifunga tano bora na alama 20.

Image: CHELSEA

Hatimaye ligi ya kandanda inayoshabikiwa zaidi duniani ya EPL imerejea baada ya wiki mbili za mapumziko ya kitaifa.

Siku ya Jumamosi mashindano ya EPL yaliingia katika raundi ya 12 ambapo mechi nane zilichezwa katika nyanja mbalimbali nchini Uingereza.

Mechi ya ufunguzi ilikuwa kati ya washindi wa EPL mwaka wa 2016 Leicester City na washindi wa Champions League msimu uliopita Chelsea.

Vijana wa Thomas Tuchel waliendeleza fomu yao nzuri huku wakipata ushindi wa 3-0 ugenini, matokeo ambayo yaliwasukuma alama nne kileleni.

Mechi sita zaidi zilichezwa mwendo wa saa kumi na mbili jioni ambapo mabao mengi yalishuhudiwa.

Masaibu yaliendelea kuandama Mashetani Wekundu katika ziara yao  ya Vicarage Road ambapo Watford iliwaadhibu kwa mabao 4-1 na kuongeza shinikizo kwa kocha Ole Gunnar  Solskjaer ambaye alipigwa kalamu siku ya Jumapili kufuatia msururu wa matokeo mabaya.

Joshua King, Ismaila Sarr,Joao Pedro na Emmanuel Dennis walifungia Watford bao moja kila mmoja huku Donny Van de Beek akifungia United bao la pekee. Nahodha wa United Harry Maguire alilazimika kuenda kuoga mapema baada  ya kuonyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 69 baada ya kumchezea vibaya Tom Cleverly.

Mechi kati ya Burnley na Crystal Palace na ile ya Newcastle dhidi ya Brentford ziliishia sare ya 3-3 huku Wolves wakipata ushindi wa 1-0 dhidi ya Westham. Norwich waliandikisha ushindi wao wa pili msimu huu na kuongeza nafasi yao ya kuepuka kubanduliwa nje ya EPL mwishoni wa msimu  wa 2021/22.

Mechi ya mwisho siku ya Jumamosi ilikuwa kati ya Liverpool na Arsenal ambayo ilichezwa ugani Anfield.

Wanabunduki walipoteza mechi yao ya nne msimu huu baada ya kulazwa mabao manne bila jawabu katika mechi hiyo iliyochezwa mwendo wa saa mbili unusu usiku.

Sadio Mane, Mohammed Salah, Diogo Jota na Takumi Minamino walifunga bao moja moja kila mmoja na kusukuma The Reds katika nafasi ya pili na alama 25.

Mechi mbili zilichezwa siku ya Jumapili

Washindi wa EPLmsimu uliopita walionyesha makali dhidi ya Everton na kuandikisha ushindi wa 3-0 ugani Etihad. Raheem Sterling, Rodri na Bernando Silva walifanikisha ushindi huo uliosukuma vijana wa Pep Guardiola hadi nafasi ya pili na alama 26.

Tottenham walikaribisha Leeds ugani Tottenham Hotspur Stadium mida ya saa moja unusu usiku na kupata ushindi wa 2-1. Mabao ya Spurs yalifungwa na Pierre-EmileHojbjerg na Serge Regulion huku Daniel James akifunga bao la pekee la Leeds.

Kwa sasa The Blues wanaendelea kuongoza jedwali na alama 29, City inafuata na 26, Liverpool ya tatu na alama 25, West Ham ya nne na 23 huku wanabunduki wakifunga tano bora na alama 20.

Nafasi tatu za mwisho zinashikiliwana Burnley (9), Norwich (8) na hatimaye Newcastle inafunga mkia na alama  6

View Comments