In Summary

• Muungano wa vilabu vya soka la Ulaya, UEFA unatarajiwa kuafikia maamuzi ya kuvua jiji la Saint Petersburg, huko Urusi haki ya kuwa mwenyeji wa fainali za klabu bingwa barani Ulaya.

• Tangazo hili linatarajiwa kutolewa rasmi Ijumaa 25, kutokana na mzozo wa kiusalama unaoendelea baina ya Urusi na Ukraine.

kombe la ligi ya mabingwa

Muungano wa vilabu vya soka la Ulaya, UEFA unatarajiwa kuafikia maamuzi ya kuvua jiji la Saint Petersburg, huko Urusi haki ya kuwa mwenyeji wa fainali za klabu bingwa barani Ulaya za mwaka wa 2022 kutokana na mzozo wa kiusalama unaondelea baina ya Urusi na Ukraine.

Uwanja wa Krestovsky ambao ndio uliandaa fainali za kombe la dunia za 2018 ulitarajiwa kuandaa fainali za klabu bingwa barani Ulaya za mwaka huu mnamo Mei 28, baada ya kuvuliwa haki hiyo mwaka jana kutokana na maambukizi ya virusi vya Corona kuongezeka.

Katika kikao kilichoandaliwa na kamati ya UEFA Alhamisi 24 baada ya Urusi kushambulia Ukraine, kamati hiyo iliitisha kikao kufanyika Ijumaa 25 na kujadili mipango ya kubadilisha fainali hizo kutoka Urusi kuenda taifa lingine kwa sababu za kiusalama.

Rais Vladimir Putin wa Urusi alipuuzilia mbali onyo kutoka kwa mataifa mbalimbali ya Ulaya dhidi ya kuanzisha mashambulizi dhidi ya Ukraine na kusema kwamba mashambulizi yao dhidi ya Ukraine yataendelea na taifqa lolote litakaloingilia mgogoro huo litaona cha mtema kuni.

Kutokana na ripoti zilizotumwa kwa ESPN, muungano huo wa UEFA unatazamia kuanzisha mchakato wa kutafuta uga mbadala wa kuandaa fainali hizo huku uwanja wa Wembley nchini Uingereza ukijiondoa katika kinyang’anyiro cha kupigania nafasi hiyo kwa sababu tayari ushaifadhiwa kwa mchujo wa mashindano ya EFL.

Vile vile shirikisho la soka duniani FIFA pia lianaendelea kutathmini hali ilivyo kati ya Urusi na Ukraine huku nchi ya Urusi ikitarajiwa kucheza katika mechi ya mchujo dhidi ya Poland mwezi ujao nayo Ukraine ikitarajiwa kucheza dhidi ya Scotland.

View Comments