In Summary

•Wachezaji 3 waliosajiliwa mwezi Januari, Joao Felix, Enzo Fernandez na Mykhailo Mudryk, walijumuishwa kwenye orodha mpya.

• Aubameyang hata hivyo alifanywa mwana-kondoo wa dhabihu ili kuwafungulia njia wachezaji wapya.

Mshambuliaji wa Chelsea Pierre-Emerick Aubameyang
Image: HISANI

Klabu ya Chelsea iliwasilisha orodha mpya ya kikosi cha Ligi ya Mabingwa siku ya Ijumaa kufuatia kufungwa kwa dirisha la uhamisho la Januari mnamo Januari 31.

"Kufuatia kufungwa kwa dirisha la usajili la Januari, Orodha ya A ya wachezaji wa hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa 2022/23 imewasilishwa," taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti rasmi ya The Blues ilisoma.

Wachezaji watatu mahiri waliosajiliwa mwezi Januari, Joao Felix, Enzo Fernandez na Mykhailo Mudryk, walijumuishwa kwenye orodha mpya iliyowasilishwa na klabu ya London.

Nahodha wa zamani wa Arsenal Pierre- Emerick Aubameyang hata hivyo alifanywa mwana-kondoo wa dhabihu ili kuwafungulia njia wachezaji wapya.

Kikosi kipya sasa kinajumuisha; Makipa (Kepa Arrizabalaga, Marcus Bettinelli, Edouard Mendy),  Walinzi (Thiago Silva, Trevoh Chalobah, Ben Chilwell, Reece James, Kalidou Koulibaly, Cesar Azpilicueta, Marc Cucurella, Wesley Fofana, Viungo wa kati (Enzo Fernandez, N'Golo Kante, Mateo Kovacic, Christian Pulisic, Ruben Loftus-Cheek, Raheem Sterling, Mason Mount, Denis Zakaria, Hakim Ziyech, Conor Gallagher, Carney Chukwuemeka),  na Washambuliaji (Joao Felix, Mykhailo Mudryk, Kai Havertz).

Aubameyang amekuwa na msimu mgumu  baada ya kusajiliwa na The Blues mwezi Septemba mwaka jana. Uhamisho huo ulionekana tatani kwani miezi michache kabla alikuwa nahodha wa mmoja wa wapinzani wakuu wa Chelsea, Arsenal.

Haijabainika kwa nini mchezaji huyo wa kimataifa wa Gabon ndiye alichaguliwa kuondolewa kwenye kikosi lakini meneja, Graham Potter amedokeza kwamba mchezo wake katika klabu hiyo bado haujaridhisha.

"Pierre hajafanya kosa hata kidogo, hakuna shida. Ni bahati mbaya tu na Aubameyang atapigania nafasi yake hadi kipindi cha msimu kilichosalia," Graham Potter alisema kwenye mahojiano ya Ijumaa jioni.

Aubameyang aliondoka Arsenal na kujiunga na Barcelona takriban mwaka mmoja uliopita baada ya kutofautiana na meneja wa Wanabunduki, Mikel Arteta na kupoteza nafasi yake kwenye kikosi.

Mwezi  Septemba, klabu hiyo ya Uhispania ilimuuza kwa Chelsea, uhamisho ambao uliwakera sana mashabiki wa Arsenal.

View Comments