In Summary

• Awali mchezo huo ulisimama kwa takriban dakika 20 kutokana na pingamizi la viongozi wa El Suez waliomtaka mwamuzi kuangalia goli kwenye kioo cha simu ya mkononi.

• Mechi iliyoisha kwa ushindi wa mabao 3-1 kwa Montakhab El-Suez.

Mwamuzi akipitia bao kwenye kioo cha simu ya mkononi
Image: Hisani

Kamati ya waamuzi ya Shirikisho la Soka la Misri (EFA) iliamua Jumanne kumsimamisha kwa muda usiojulikana mwamuzi wa mchezo kati ya Montakhab El-Suez na El-Nasr katika mchezo wa ligi daraja la pili siku ya Ijumaa.

Inaarifiwa kwamba refa huyo alitumia video iliyorekodiwa katika simu ya shabiki mmoja na kuitumia kama kigezo cha kufuta bao la El-Nasr kwa madai kwamba lilikuwa bao la kuotea.

“Mwamuzi alighairi bao la El-Nasr baada ya kuangalia skrini ya simu ya rununu kuthibitisha mchezaji wa El-Nasr aligusa mpira kwa mkono wake kabla ya kufunga bao,” sehemu ya taarifa ya madai hayo ilisoma.

Picha zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii ya Misri zikimuonyesha mwamuzi akiangalia goli kwenye skrini ya simu ya mkononi, jambo lililosababisha dhihaka za watazamaji.

Kulingana na afisa wa Montakhab El-Suez, tukio lilianza wakati mchezaji wa El-Nasr alipoifungia timu yake bao la kusawazisha huku matokeo yakiwa 2-1 kwa upande wa timu El Suez.

Awali mchezo huo ulisimama kwa takriban dakika 20 kutokana na pingamizi la viongozi wa El Suez waliomtaka mwamuzi kuangalia goli kwenye kioo cha simu ya mkononi.

Mwamuzi alikubali pendekezo hilo na alifuta bao baada ya kukagua eneo la tukio.

Uamuzi huo uliibua hasira za viongozi wa El-Nasr na mchezo ukasimama kwa dakika nyingine 15 kabla ya kuendelea na mechi iliyoisha kwa ushindi wa mabao 3-1 kwa Montakhab El-Suez.

Mapema wiki hii, kamati ya mashindano ya EFA iliridhia matokeo ya mchezo huo na kuwatoza faini maafisa kadhaa wa vilabu vyote viwili.

View Comments