In Summary

Rubiales alisimamishwa na Fifa siku ya Jumamosi baada ya Hermoso kusema busu kabla ya timu kunyanyua kombe haikuwa ya makubaliano.

Kocha mkuu wa Uhispania aliyeshinda Kombe la Dunia la Wanawake Jorge Vilda amemkosoa rais wa shirikisho la kandanda aliyesimamishwa Luis Rubiales, akitaja wakati alipombusu mchezaji Jennifer Hermoso "haufai na haukubaliki".

Rubiales alisimamishwa na Fifa siku ya Jumamosi baada ya Hermoso kusema busu kabla ya timu kunyanyua kombe haikuwa ya makubaliano.

Wakufunzi wote wa Vilda wamejiuzulu katika maandamano dhidi ya Rubiales, lakini Vilda mwenyewe hajajiuzulu licha ya maoni yake ya hivi karibuni.

Kocha huyo alionekana akipiga makofi kwenye mkutano mkuu usio wa kawaida wa shirikisho la Uhispania siku ya Ijumaa, wakati Rubiales alipotoa hotuba ya msisitizo ambapo alisisitiza mara kwa mara kuwa hatajiuzulu na kudai kuwa yeye ni mwathiriwa.

Wawili hao walikuwa washirika baada ya Rubiales kusimama na Vilda mnamo Septemba 2022 wakati wachezaji 15 wa timu ya taifa walipojiondoa kwenye kikosi, wakisema kuwa usimamizi wa meneja huyo ulikuwa unaathiri hali yao ya kihisia na afya.

Vilda alitoa taarifa Jumamosi usiku, akisema: "Nasikitika sana kwamba ushindi wa soka la wanawake wa Uhispania umeathiriwa na tabia isiyofaa ambayo kiongozi wetu mkuu hadi sasa, Luis Rubiales, ameifanya na ambayo yeye mwenyewe ameitambua.

“Hakuna shaka kuwa haikubaliki na haiakisi kabisa kanuni na maadili ninayotetea katika maisha yangu, kimichezo kwa ujumla na hasa katika soka.

Fifa imemsimamisha kwa muda Rubiales, 46, mchezaji wa zamani wa La Liga wa Levante, kujihusisha na soka kwa siku 90.

Serikali ya Uhispania pia imeanza taratibu za kisheria huku ikilenga kumsimamisha kazi.

 

 

 

View Comments