In Summary

•Ilikuwa ni wakati akiitambulisha Simba SC ya Tanzania ambapo alizungumza lugha ya Kiswahili na kuwasisimua maelfu ya mashabiki.

•Bosi huyo wa FIFA aliitaja Ligi hiyo mpya ya Soka ya Afrika kuwa mashindano bora zaidi ya kandanda barani Afrika 

Rais wa FIFA Gianni Infantino aliwasisimua mashabiki wa soka kwa ujuzi wake wa Kiswahili Ijumaa.
Image: HISANI

Rais wa FIFA Gianni Infantino aliwasisimua mashabiki wa soka kwa Kiswahili chake siku ya Ijumaa wakati akitoa hotuba yake kwenye sherehe za ufunguzi wa Ligi ya Soka ya Afrika (AFL) kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, Tanzania.

Infantino alikuwa miongoni mwa wageni mashuhuri wa kimataifa waliopamba hafla ya ufunguzi wa ligi hiyo mpya ya Afrika ambayo inatazamiwa kubadilisha soka la klabu barani.

Rais alipongeza Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) kwa juhudi zake za kuandaa ligi ya kandanda akiitaja kuwa ushahidi wa dira na kujitolea kwao katika mchezo huo unaopendwa na mabilioni ya mashabiki kote duniani.

"Nataka kumshukuru Rais wa CAF, Patrice Motsepe, na soka zima la Afrika kwa juhudi zao za kuendeleza soka barani Afrika," alisema Bw Infantino kwa Kiingereza.

Rais huyo wa FIFA pia alitambua vilabu viwili vilivyokuwa vifungue shindano hilo, Simba SC ya Tanzania na Al Alhy ya Algeria.

Ilikuwa ni wakati akiitambulisha Simba SC ya Tanzania ambapo alizungumza lugha ya Kiswahili na kuwasisimua maelfu ya mashabiki waliokuwa wamekusanyika uwanjani.

“Simba nguvu moja!! Simba nguvu moja!!” Infantino alisema kwa Kiswahili mashabiki wakishangilia na kuinua mabango ya Simba.

Aliendelea, “Karibu Tanzania.. huu ni upendo, huu ni upendo, hii ni Tanzania, hii ni Afrika, hii ni Simba, hii ni Al Ahly, hii ni CAF, hii ni FIFA na hii ni mpira. Soka inaunganisha dunia na leo soka inaunganisha dunia kutoka Tanzania.”

Bosi huyo wa FIFA aliitaja Ligi hiyo mpya ya Soka ya Afrika kuwa mashindano bora zaidi ya kandanda barani Afrika na fursa nzuri kwa vilabu vya Kiafrika kuwa katika medani ya kandanda ya kimataifa.  Aliwaomba Waafrika kufurahia shindano hilo kwani linaanza safari inayotarajiwa kuwa ya kuvutia.

Alimalizia hotuba yake kwa kusema , “Asante sana!” kwa lugha ya Kiswahili.

View Comments