In Summary

• "Unapomzungumzia Cristiano Ronaldo, unamzungumzia mmoja wa wachezaji bora zaidi duniani," Olunga alimpa maua Ronaldo.

Olunga na Ronaldo
Image: Instagram

Ligi ya mabingwa katika vilabu vya mataifa ya bara Asia itaendelea usiku wa leo Jumanne ambapo timu ya nahodha wa Kenya, Michael Olunga, Al Duhail ya Qatar itasafirisha kwenda nchini Saudi Arabia kuchuana na timu ya nahodha wa Ureno Christiano Ronaldo, Al Nassr.

Mchezo huo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Al Awal Park Oktoba 24, utakuwa ni mchezo wa tatu wa hatua ya makundi kwa pande zote mbili huku mbio za kuwania kufuzu kwa raundi inayofuata zikipamba moto.

Kwa sasa Al-Nassr ya Ronaldo inaongoza kundi hilo la timu nne ikiwa na pointi 6 baada ya kuzishinda Persepolis na Istiqlol Dushanbe. Al-Duhail, bado hawajashinda mchezo wowote baada ya kutoka sare na Istiqlol kabla ya kushuka dimbani Persepolis. Wanashika nafasi ya tatu kwenye msimamo.

Timu iliyo katika nafasi ya kwanza pekee ndiyo itafuzu baada ya kumalizika kwa hatua ya makundi.

Upande wa Al Duhail wanajivunia talanta kama Olunga na Phillipe Coutinho huku wenzao Al Nassr wakijivunia mastaa kama Ronaldo na Mane miongoni mwa wengine.

Akizungumza na vyombo vya habari kuelekea mpambano wa leo, Olunga alimmiminia sifa Ronaldo lakini akasisitiza kwamba lengo lao kuu ni kuishinda timu hiyo inayoongozwa na Mreno huyo mwiba kwa walinda lango.

"Unapomzungumzia Cristiano Ronaldo, unamzungumzia mmoja wa wachezaji bora zaidi duniani, na kwangu ni heshima kucheza naye kwenye uwanja mmoja...lakini lengo letu kesho ni kushinda mechi."

View Comments