Hafla ya 67 ya Ballon d’Or ilifanyika usiku wa Jumatatu, Oktoba 30 kwenye ukumbi wa Théâtre du Châtelet jijini Paris, Ufaransa ambapo kulikuwa na washindi tofauti katika vipengele mbalimbali.
Staa wa soka wa Argentina, Lionel Messi alishinda taji la Ballon d’Or kwa Wanaume kwa mara ya nane katika maisha yake ya soka baada ya kupata mafanikio makubwa katika mwaka mmoja uliopita. Mshambuliaji huyo matata mwenye umri wa miaka 36 hapo awali aliwahi kushinda tuzo hiyo mwaka wa 2009, 2010, 2011, 2012, 2015, 2019 na 2021.
Erling Haaland wa Manchester City na Norway aliibuka wa pili huku staa wa PSG na Ufaransa, Kylian Mbappe akishika nafasi ya tatu. Wengine walioingia kwenye orodha ya kumi bora ni Rodri wa Manchester City, Vinicius Junior wa Real Madrid, Julian Alvarez wa Manchester City, Victor Osimhen wa Napoli, Bernardo Silva wa Manchester City na Luka Modric wa Real Madrid.
Kiungo wa kati wa timu ya wanawake ya Barcelona, Aitana Bonmati kwa upande mwingine alishinda Tuzo ya Ballon d’Or ya Wanawake 2023, ikiwa ni mara ya kwanza kwa Mhispania huyo kushinda taji hilo la kifahari. Bonmati alikuwa katika timu ya Wanawake ya Uhispania iliyoshinda Kombe la Dunia la Wanawake 2023 mapema mwaka huu.
Katika vipengele vingine, Manchester City ilishinda tuzo ya klabu bora ya mwaka wa 2023 ya Wanaume huku Barcelona Women ilishinda Klabu ya Wanawake ya mwaka.
Staa wa Real Madrid na Uingereza, Jude Bellingham alitunukiwa tuzo la Kopa Trophy 2023 huku kipa wa Argentina na Aston Villa Emiliano Martinez akinyakua Yachine Trophy kwa kipa bora.
Vinicius Mdogo wa Real Madrid na Brazil pia alitunukiwa tuzo ya Socrates wakati wa Sherehe za 67 za Ballon d'Or huko Paris, Ufaransa Jumatatu usiku.