In Summary

•Mchezaji huyo wa Napoli mwenye umri wa miaka 24 alinyakua tuzo katika tuzo za Shirikisho la Soka Afrika (Caf) Jumatatu usiku.

•Kupanda kwa Osimhen hadi kileleni kumekuwa safari ya polepole badala ya simulizi ya kuchipukia ghafla kwa njia ya ajabu .

Image: BBC

Victor Osimhen amesifiwa kama "mfalme mpya wa Afrika" baada ya mshambuliaji huyo wa Nigeria kutangazwa kuwa Mwanasoka Bora wa Mwaka wa Bara la Afrika kwa 2023.

Mchezaji huyo wa Napoli mwenye umri wa miaka 24 alinyakua tuzo katika tuzo za Shirikisho la Soka Afrika (Caf) Jumatatu usiku, akishindana na nahodha wa Misri, Mohamed Salah na mlinzi wa Morocco Achraf Hakimi.

Kwa Osimhen, ambaye alikulia kwenye mitaa yenye vumbi ya Olusosun huko Lagos, ni "ndoto iliyotimia" baada ya kukabili hali halisi ya maisha akiwa mtoto.

"Lazima nimshukuru kila mtu ambaye amenisaidia katika safari hii na Waafrika wote ambao wamesaidia kuniweka kwenye ramani licha ya kasoro," Osimhen alisema.

Akilakiwa kila siku na uvundo kutoka kwa jalala katika mtaa wake, Osimhen anasema alikuwa na hamu kubwa ya kufanikiwa dhidi ya uwezekano wowote.

Ilimbidi kuuza magazeti na maji ya chupa akielezea hali yake kuwa "ya uchochole'

"Kama mvulana mdogo ambaye ilibidi atembee kwenye misongamano ya magari karibu kila siku ili kustahimili changamoto nyingi ambazo mimi na familia yangu tulikuwa tunakabiliana nazo, kuwa nyota mwenye thamani barani Afrika na katika kandanda ya ulimwengu ilikuwa ndoto isiyowezekana," alisema katika ujumbe uliotumwa kwenye X.

"Safari yangu ya soka imekuwa ya panda shuka nyingi .

"Mabao na shangwe za ushindi hunifanya niendelee hata wakati wakosoaji, chuki na maumivu ya kushindwa yanaponipiga sana kifuani."

Baada ya kufunga mabao 26 na kuisaidia Napoli kutwaa taji la kwanza la ligi ya Italia katika kipindi cha miaka 33, Osimhen amekuwa Mnigeria wa kwanza kushinda tuzo ya Caf ya wanaume tangu fowadi wa zamani wa Arsenal Nwankwo Kanu mwaka 1999.

"Alichofanya Osimhen ni cha ajabu," mshambuliaji wa zamani wa Arsenal na Togo Emmanuel Adebayor, ambaye alishinda tuzo hiyo mwaka wa 2008, aliiambia Caf TV.

"Kufunga mabao kunaweza kuwa rahisi Uingereza lakini kufanya hivyo nchini Italia sio rahisi kwa sababu wana ulinzi mkali na mbinu zenye nguvu'.

Huku mshambuliaji wa zamani wa Ivory Coast, Didier Drogba, ambaye pia ni Mwanasoka Bora wa Mwaka wa Caf mara mbili, akimtaja mshambuliaji huyo wa zamani wa Lille kama nyota mpya wa kifalme mpya katika kandanda barani Afrika, sasa kuna matumaini kwamba anaweza kuisaidia Nigeria kwenye enzi mpya ya mafanikio.

Mtoto wa hatima

Osimhen (kushoto) aliingia ulingoni kwenye Kombe la Dunia la Fifa la Vijana wasiozidi umri wa miaka 17 mwaka 2015.
Image: BBC

Kupanda kwa Osimhen hadi kileleni kumekuwa safari ya polepole badala ya simulizi ya kuchipukia ghafla kwa njia ya ajabu .

Akiwa katika kikosi cha Nigeria katika Kombe la Dunia la U-17 na ushindi wao mwaka wa 2015 ilikuwa ni hatua ya mabadiliko katika maisha yake ambayo ilionyesha kuwa alikuwa 'mtoto wa hatima'.

Mabao yake 10 akiwa Chile yalimwezesha kutwaa kiatu cha dhahabu /mfungajaji wa mabao mengi na kumfanya kuwa mchezaji bora chipukizi wa mwaka wa Caf - lakini Osimhen nusura akose uteuzi wa kikosi hicho.

"Tayari nilikuwa nimempuuza kwa sababu alijumuishwa na wachezaji wengine waliocheza vibaya," Emmanuel Amunike, kocha wa timu hiyo, aliambia BBC Sport Africa.

"Lakini wahudumu wangu wa kiufundi walimwona na wakavuta hisia zangu kwake. Nilimpa nafasi nyingine na akajidhihirisha kuingia kikosi hicho."

Haikushangaza kwamba Osimhen, baada ya kupokea tuzo yake ya Caf siku ya Jumatatu nchini Morocco, alimsifu kocha wake wa zamani kwa kumsaidia kutimiza ndoto zake.

"Shukrani za kipekee zimwendee Emmanuel Amunike. Bila yeye, sidhani kama ningekuwa nimesimama hapa nikishikilia moja ya tuzo kuu katika soka la dunia," alisema.

Hakika kumekuwa na matuta machache njiani.

Uhamisho wake kwa klabu ya Ujerumani ya Wolfsburg mnamo Januari 2017 nusura ugeuke kuwa ndoto mbaya kwa chipukizi huyo, ambaye alicheza mara 16 bila kufunga kabla ya kuhamia Charleroi ya Ubelgiji kwa mkopo 2018-19 na kupata njia ya kumpa fursa nyingine katika soka.

Sifa ya Osimhen iliimarishwa akiwa na Lille hadi Napoli iliripotiwa kulipa $96m (euro 81.3m) - moja ya ada za juu zaidi kuwahi kutokea kwa mchezaji wa Kiafrika - kwa huduma yake mnamo Julai 2020.

Kabla ya msimu wake mzuri ambao alinyakua taji la kihistoria la Serie A, alilazimika kukosa kushiriki Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2021 kwa sababu ya Covid-19 na jeraha la uso ambalo bado linamhitaji kucheza akiwa amevaa barakoa.

Kwa kuongezea, ilibidi ashughulikie kifo cha mama na baba yake mnamo 2020

"Kuwapoteza wazazi wangu wapendwa katika safari hii kunaacha kovu moyoni mwangu kwani wamekuwa ndio nguvu yangu kuu ya mafanikio," Osimhen aliongeza katika chapisho lake kwenye X.

"Kwa familia yangu nzuri, asanteni kwa kunijali kila wakati na kunipenda sana. Nisingeweza kufika hapa bila msaada wenu"

Enzi mpya kwa soka ya Afrika?

Osimhen alihusika moja kwa moja katika kufunga mabao 31 wakati Napoli ikishinda Serie A na kufika robo fainali ya Uefa Champions League msimu uliopita.
Image: BBC

Mshambulizi wa Liverpool, Salah na mchezaji wa zamani wa Reds Sadio Mane, wote wenye umri wa miaka 31, walikuwa wameshinda tuzo nne zilizopita za Caf kati yao, na mafanikio ya Osimhen huko Marrakesh yanaweza kutangaza ujio wa kizazi kijacho.

mwenzake wa Super Eagle Victor Boniface (Bayer Leverkusen), kiungo wa kati wa Ghana Mohammed Kudus (West Ham) na mshambuliaji wa Guinea, Serhou Guirassy (Stuttgart) wote tayari wameshaanza msimu huu.

Wakati huo huo, mashabiki wa Nigeria wanatumai kutambuliwa kwa Osimhen kunaweza kutoa msukumo kwa timu ya taifa kutinga tena kombe la Afcon, ambalo Wenyeji hao wa Afrika Magharibi walilinyanyua mara ya mwisho mwaka 2013.

Timu hiyo ilishindwa kufuzu kwa fainali hizo mnamo 2015 na 2017, ilimaliza nafasi ya tatu mnamo 2019 na kutolewa katika hatua ya 16 bora katika toleo la 2021 nchini Cameroon.

"Kutambuliwa huku kwa kiwango cha juu ni risasi kubwa kwa mpira wa miguu wa Nigeria," mwenyekiti wa Chama cha Soka cha Abuja Adam Muktar Mohammed aliambia AFP.

"Ni dhahiri, kuna vipaji vingi nchini Nigeria. Inatubidi tu kutumia talanta hii kuwa nguvu kuu katika soka ya kimataifa."

Drogba - ambaye Osimhen amemkubali kama mfano wake akikua - anaamini Nigeria inaweza kuwa tishio kwenye Afcon 2023, ambayo itaanza nchini Ivory Coast mwezi ujao.

Super Eagles wamepangwa pamoja na wenyeji, Equatorial Guinea na Guinea-Bissau katika Kundi A kwenye fainali.

"Tunakusubiri Januari," Drogba aliongeza katika ujumbe wake wa pongezi kwa Osimhen.

Iwapo Osimhen atatwaa taji la Kombe la Mataifa ya Afrika mjini Abidjan tarehe 11 Februari, sifa alizopata nchini Nigeria yenye mapenzi makubwa ya soka tangu kutawazwa kwake Jumatatu usiku zitasogezwa katika viwango vipya.

View Comments