In Summary

• Mechi kati ya Nigeria na Equatorial Guinea iliisha kwa sare ya 1-1 huku mabao yote mawili yakifungwa kipindi cha kwanza.

•Mechi nyingine tatu zitachezwa siku ya Jumatatu jioni, Januari 15 huku mashindano ya AFCON yakiingia siku ya tatu.

Mechi kati ya Misri na Mozambique iliishia sare ya 2-2.
Image: AFCON

Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2023  (AFCON) yaliingia siku ya pili mnamo Jumapili, Januari 14, huku mechi tatu zikichezwa kwa nyakati tofauti jioni.

Timu ya Nigeria ilimenyana na Equatorial Guinea katika mechi ya ufunguzi iliyochezwa kuanzia saa kumi na moja jioni. Mechi hiyo ya kusisimua iliisha kwa sare ya 1-1 huku mabao yote mawili yakifungwa kipindi cha kwanza.

Mshambulizi wa Equatorial Guinea Iban Salvador alikuwa wa kwanza kuzifumania nyavu dakika ya 36 kabla ya mshambuliaji matata wa Napoli Victor Osimhen kuisawazishia Nigeria dakika mbili tu baadaye.

Mechi kati ya Misri na Msumbiji iliyochezwa majira ya saa mbili usiku nayo pia iliishia kwa sare huku timu zote zikifungana mabao mawili kila moja.

Msumbiji ilikuwa karibu kushinda mechi hiyo baada ya kufunga mabao mawili ya haraka katika dakika ya 55 na 58 kabla ya nyota wa Liverpool, Mo Salah kuisawazishia Misri kwa mkwanju wa penalti katika dakika ya 97. Misri walikuwa wamepata bao la kuongoza mapema katika mechi hiyo huku mshambuliaji Mostafa Mohamed akifunga bao la kwanza katika dakika ya 2 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Mo Salah.

Mechi ya tatu ilishuhudia Cape Verde ikishinda 2-1 dhidi ya Ghana ambayo imepigiwa upato sana. Viungo Jamilo Monteiro na Garry Rodrigues walifunga mabao mawili ya Cape Verde huku beki wa Fernebahce Alexander Djiku akifunga bao pekee la Ghana baada ya kupata pasi nzuri kutoka kwa Jordan Ayew wa Crystal Palace.

Mechi nyingine tatu zitachezwa siku ya Jumatatu jioni, Januari 15 huku mashindano ya AFCON yakiingia siku ya tatu.

Tazama ratiba ya Jumatatu ya AFCON 2023;

KUNDI C: Senegal vs Gambia –Charles Konan Banny Stadium, Yamoussoukro (Saa kumi na moja jioni masaa ya Afrika Mashariki)

KUNDI C: Cameroon vs Guinea- Charles Konan Banny Stadium, Yamoussoukro (Saa mbili jioni masaa ya Afrika Mashariki)

KUNDI D: Algeria vs Angola- Stade de la Paix, Bouake ((Saa tano jioni masaa ya Afrika Mashariki)

View Comments