logo

NOW ON AIR

Listen in Live

AFCON 2023: Tanzania yapokwa ‘tonge mdomoni’ na Zambia

Hii ni sare ya pili kwa Tanzania katika michuano ya AFCON.

image
na Samuel Maina

Michezo22 January 2024 - 04:09

Muhtasari


  • •Bao la dakika ya 88 la Zambia limefuta matumaini ya Tanzania kuandikisha ushindi wa kwanza katika michuano ya Afcon.
  • •Hii ni sare ya pili kwa Tanzania katika michuano ya AFCON.

Bao la dakika ya 88 la Zambia limefuta matumaini ya Tanzania kuandikisha ushindi wa kwanza katika michuano ya kombe la mataifa ya Afrika (Afcon).

Tanzania iliandikisha goli la kwanza katika dakika ya 11 kupitia winga wake wa kimataifa Simon Msuva akiunganisha pasi maridhawa kutoka kwa nahodha Mbwana Samatta.

Zambia ilipata pigo kwa kutolewa kwa kadi nyekundu kwa nahodha wao Rodrick Kabwe katika dakika ya 44.

Tanzania iliendelea kuutawala mchezo huo na kukosa nafasi kadhaa za wazi kuongeza goli la pili wakati Zambia ikicheza mchezo wa kujilinda zaidi na kufanya mashambulizi ya kushtukiza.

Mashambulizi hayo ya kushtukiza yalizaa matunda katika dakika ya 88 ambapo mshambuliaji wa klabu ya Leicester City ya England Patson Daka alipofunga bao la kusawazisha kwa kichwa kikali akiunganisha krosi ya Clatous Chota Chama anayechezea klabu ya Simba ya Tanzania.

Hii ni sare ya pili kwa Tanzania katika michuano ya AFCON. Sare ya kwanza waliipata kwa Ivory Coast katika michuano ya mwaka 1980 ambapo magoli yalikuwa 1-1. Katika michuano ya mwaka 2019 Tanzania ilipoteza michezo yote mitatu.

Kwa matokeo hayo sasa Tanzania inaendelea kushikilia mkia wa kundi Fwakiwa na alama moja huku Zambia na DRC wakiwa na alama mbili kila mmoja na kinara wa kundi ni Morocco wenye alama nne. Morocco na DRC walitoka sare ya 1-1 katika mchezo wa awali wa kundi hilo.

Tanzania sasa itaminyana na DRC siku ya Jumatano katika mchezo wa mwisho wa makundi, Morocco na Zambia pia wataminyana siku hiyo. Mpaka sasa hakuna timu yoyote katika kundi hilo ambayo imekata tiketi ya kucheza katika hatua ifuatayo


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved