In Summary

•Ochieng amesafiri kuelekea Malawi kujiunga na kambi ya Harambee Stars baada ya kupokea mwito kutoka kwa  kocha Engin Firat.

•Ochieng amechezea Harambee Stars mechi yake ya mwisho Juni 2023,kwenye mashindano ya mataifa manne kabla ya kutemwa nje kwenye kikosi.

David Ochieng
Image: Instagram

David ‘Cheche’ Ochieng ambaye ni beki wa timu ya Kenya Police Fc atajiunga na kikosi cha Harambee Stars nchini Malawi baada ya kuitwa na kocha Engin Firat.

Ochieng atakuwa mchezaji wa hivi punde zaidi kujiunga na kambi kuimarisha safu ya ulinzi ya Kenya kwa mechi ya kufuzu kwa kombe la dunia 2026  dhidi ya mabingwa wa Afrika Ivory Coast itakayochezwa Jumanne katika uwanja wa kitaifa wa Bingu mjini Lilongwe.

Beki huyo amechezea Harambee Stars mechi  kadhaa hapo awali kabla ya kutemwa nje kwenye kikosi kilichosafiri kwenda Malawi. Mechi yake ya mwisho ikiwa ni Juni 2023 alipocheza katika mashindano ya mataifa manne katika mechi dhidi ya Pakistan na Mauritius.

Firat alitaja kuwa sare dhidi ya Burundi ilitokana na majeraha ambayo yanakumba kikosi chake. Beki maarufu Erick 'Marcelo' Ouma yupo mkekani pamoja na Joseph Okumu, hivo ana imani kuwa David Ochieng atakuwa anaimarisha ulinzi kwenye kikosi cha Harambee Stars.

Firat amewajumuisha wachezaji kadhaa  tangu mechi dhidi ya Burundi kukamilika,miongoni mwao wakiwa ni David Okoth kutoka klabu ya Kenya Police, Baron Ochieng anayechezea Sofapaka pamoja na Clyde Senaji anayechezea Nyasa Big Bullets nchini Malawi.

Kenya itakuwa inashuka dimbani Jumanne 11, Juni 2024 kumenyana na vigogo wa Afrika Ivory Coast kwenye mechi yao ya pili mwezi huu baada ya kukabana sare ya 1-1 na Burundi.

IKiwa Harambee stars watakosa alama tatu Jumanne, basi matumaini ya kufuzu kwa kombe la dunia yatakuwa yanadidimia kwa kuwa watakuwa alama nane nyuma ya viongozi wa jedwali, Ivory Coast.

Je,unahisi kuwa Harambee Stars watafuzu kwenye kombe la dunia 2026

View Comments