In Summary

•Steve Cooper amejiunga na Leicester City kama kocha mkuu kwa mkataba wa miaka mitatu baada ya aliyekuwa kocha wao,Enzo Maresca kuhamia Chelsea.

•Cooper alifutwa kazi na Nottingham Forest  baada ya matokeo mabovu .

Steve Cooper
Image: Ghetty images

Klabu ya Leicester imemteua meneja wa zamani wa Nottingham Forest,Steve Cooper kama kocha mkuu kwa mkataba wa miaka mitatu.

Cooper anachukua nafasi ya Enzo Maresca, ambaye aliondoka na kujiunga na Chelsea mapema msimu huu wa joto.

Mkufunzi huyo amekuwa hana kazi tangu afutwe na Nottingham Forest  Disemba mwaka jana.Hii ikiwa ni msururu mbovu wa matokeo baada ya kumaliza katika nafasi ya 17 kwenye ligi kuu ya primia ,baada ya kushinda mara moja pekee katika michezo 13.

Raia huyo wa Wales, mwenye umri wa miaka 44  pia amewahi kuwa kocha wa timu za kimataifa za U16 na U17, akishinda Kombe la Dunia mnamo 2017, kabla ya kuinoa Swansea City kutoka 2019-2021.

Leicester wataanza msimu wao wa ligi kuu ya 2024/25  dhidi ya Spurs usiku wa Jumatatu  nyumbani,mnamo Agosti 19.

Mabingwa hao,waliopandishwa daraja kisha watasafiri hadi Craven Cottage kumenyana na Fulham katika mchezo wao wa pili kabla ya kurejea King Power Stadium kuvaana na Aston Villa mnamo Agosti 31.

Derby yao ya kwanza ya East Midlands dhidi ya Nottingham Forest ambapo Cooper anaweza kukabiliana na klabu yake ya zamani itachezwa nyumbani Oktoba 26, na mchezo wa marudiano utafanyika kwenye uwanja wa City Ground Mei 10.

Meneja wao wa zamani Maresca anatarajiwa kurejea King Power Stadium na Chelsea mnamo Novemba 23. Wanakabiliwa na ratiba ngumu ya krismasi na mwaka mpya, ikiwa ni pamoja na safari ya Anfield kumenyana na Liverpool siku ya 'Boxing Day' na mchezo wa nyumbani dhidi ya Manchester City Disemba 29.

Je,Steve Cooper atawawezesha Leicester City kuendeleza fomu yao nzuri waliyokuwa nayo na Enzo Maresca ama mambo yatayumba?

View Comments