Shirikisho la kandanda humu nchini, FKF limetoa taarifa kuhusu wachezaji wanne wa Kenya kunyanganywa pasipoti zao katika ubalozi wa Italia jijini Nairobi.
Kupitia kurasa za mitandao ya kijamii, FKF ilifichua kwamba wachezaji wanne kwa majina Ben Stanley, Ronney Onyango, Musa Masika na Shariff Majabe walikwenda katika ubalozi huo kwa lengo la kufikisha maombi ya visa ya kusafiria kwenda Italia.
Hata hivyo, wanne hao hawakuwa wamepata barua kutoka kwa shirikisho bali walikuwa wameghushi barua kuonyesha kuwa walikuwa wamethibitishwa na shirikisho.
Baada ya barua hiyo kugundulika kuwa bandia, pasipoti za wanne hao zilishikiliwa.
Lakini je, walikuwa na nia ya kusafiri kuelekea Italia kwa lengo lipi?
FKF inasema uchunguzi wa awali ulionyesha kuwa kulikuwa na mchezaji wa zamani ambaye kwa sasa anaishi ughaibuni akishirikiana na afisa kutoka timu ya ligi pana ya taifa, NSL ambao walikuwa nyuma ya mpango huo.
“Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa mchezaji wa zamani ambaye kwa sasa anaishi Ughaibuni na afisa wa klabu ya NSL na maagenti wao ndio wako nyuma ya mpango wa kughushi barua ya FKF na barua za maombi ya visa. Shirikisho linaendelea kushirikiana na ubalozi wa Italia kwa dhumni la kuhakikisha wanne hao wanarejeshewa pasipoti zao,” sehemu ya taarifa hiyo ilisoma.
Kando na hilo, FKF ilitangaza kwamba tayari wameanzisha mchakato wa kinidhani wa ndani dhidi ya wanne hao huku wakisema kwamba hawatatoa taarifa nyingine zaidi hadi pale suala hilo litakapotatuliwa.