Tuzo za kuadhimisha miaka 51 ya Chama cha Wanasoka wa Kulipwa (PFA) zilifanyika mjini Salford, Manchester siku ya Jumanne jioni ambapo wachezaji mbalimbali wa Ligi Kuu ya Uingereza walitunukiwa tuzo tofauti.
Vilabu vya Arsenal na Manchester City vilitawala hafla ya tuzo hizo huku takriban tuzo zote zikichukuliwa na wachezaji wao.
Kipa David Raya, mabeki William Saliba na Gabriel Magalhaes, na viungo Declan Rice na Martin Odegaard wa Arsenal walichaguliwa kwenye timu bora ya mwaka ya Ligi ya Premia pamoja na Virgil Van Dijk wa Liverpool na Olie Watkins wa Aston Villa.
Beki Kyle Walker, kiungo wa kati Rodri, washambulizi Phil Foden na Erling Haaland wa Manchester City pia walitajwa kwenye timu bora ya mwaka.
Washindi walipigiwa kura na wachezaji.
Mshambulizi Phil Foden alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwaka wa PFA huku Cole Palmer wa Chelsea akishinda tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi wa Mwaka.
Crysencio Summervile wa West Ham, aliyekuwa akiichezea Leeds United msimu uliopita alishinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa Championship huku Bunny Shaw wa timu ya Wanawake ya Manchester City akishinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka kwa wanawake.
Wachezaji bora waliokosa tuzo hizo ni pamoja na Bukayo Saka wa Arsenal, Bruno Fernandes wa Manchester United, Mo Salah wa Liverpool na Alexander Isak wa Newcastle.