In Summary

• Uwanja mpya wa Siaya utafunguliwa mnamo tarehe 1, Januari 2025 mechi ya ufunguzi ikiwa Gor Mahia dhidi ya Yanga SC ya Tanzania.

Ambrose Rachier, Hersi Said na James Orengo walipokutana Julai 15 jijini Dar es Salaam
Image: X//James Orengo

Gavana wa kaunti ya Siaya James Orengo amedhibitisha kuwa Gor Mahia watamenyana na Yanga SC ya Tanzania siku ya kuzindua uga wa Siaya.

Kupitia ukurasa wake wa X, gavana Orengo amesema kuwa alifanya mazungumzo na rais wa klabu ya Yanga SC Eng. Hersi Said mnamo Jumatatu tarehe 16 Septemba jijini Nairobi na kuweka mikakati ya mechi hiyo kuchezwa.

Mechi kati ya mabingwa wa Kenya Gor Mahia na miamba wa soka nchini Tanzania Yanga, itachezwa mnamo tarehe 1 Januari, 2025 katika uwanja mpya wa Siaya.

Uwanja wa Siaya ni mpya na siku hiyo ya mechi baina ya Yanga na Gor utabariki uga utakapozinduliwa rasmi rasmi kutumika.

Rais wa Yanga Eng. Said amekuwa nchini Kenya kushiriki mkutano wa CAF EXCO ulioshuhudiwa pia na Rais wa shirikisho la soka barani Afrika (CAF) Patrice Motsepe.

Ujio wa Motsepe nchini ni katika uhakiki wa matayarisho ya Kenya kuandaa mashindano ya CHAN ya .waka 2025 pamoja na maandalizi ya kuwa mwenyeji wa AFCON 2027 kwa ushirikiano na Uganda na Tanzania.

Awali gavana Orengo na mwenyekiti wa Gor Mahia Ambrose Rachier walisafiri jiji la Dar es Salaam mnano tarehe 15 Julai ambapo walikutana na rais wa Yanga Eng. Said kujadili uwezekano wa Yanga kucheza na Gor Mahia siku ya ufunguzi wa uwanja wa Siaya.

Bw. Orengo alirejea jiji la Dar es Salaam tena mwezi wa nane, kwa majadiliano na afisa mkuu mtendaji wa Yanga kuhusu mchezo huo huo wa mwakani.

View Comments