In Summary

• Kocha Wambua aliongoza Ulinzi Starlets kunyakua taji la FKF Women Cup kwa mara tatu mfululizo.

Kocha Joseph Wambua
Image: HISANI

Kocha wa klabu ya kina dada inayomilikiwa na jeshi Ulinzi Starlets inayoshiriki ligi kuu ya wanawake nchini  Joseph Wambua Mwanza ameaga dunia.

Kifo cha kocha Wambua kimedhibitishwa kupitia ukurasa wa Facebook ya klabu ya Ulinzi Stars ambayo ni klabu ya wanajeshi kwa upande wa wanaume.

Mwanza maarufu kama 'Coach Klopp' ameaga dunia ghafla ijapokuwa chanzo cha kifo chake hakijabainishwa.

Klabu ya Ulinzi Stars imemsifia kocha Joseph Wambua kama kocha aliyekuwa zaidi ya kiongozi uwanjani na aliyekuza vipaji vya kandanda sio tu kwa familia ya Ulinzi Starlets pekee yake bali kwa jamii nzima ya kabumbu nchini.

Katika ukufunzi wake kwenye timu ya Ulinzi Starlets, alifanikisha kunyakua ushindi wa kombe la mashindano ya wanawake ya FKF maarufu kama FKF Women Cup mara tatu mfululizo.

Mwanza alinyakua taji la tatu la FKF Women cup wezi Julai baada ya kuishinda Kibera Soccer Ladies mabao 2 kwa 1.

Washikadau wa soka nchini ikiwemo aliyekuwa kocha wa Harambee Stars Jacob 'Ghost' Mulee, usimamizi wa ligi wa wanawake nchini na wachezaji wa kabumbu wametuma risala zao za rambi rambi.

View Comments