In Summary

•Mnamo siku ya Alhamisi, Septemba 19, FIFA ilitoa ripoti kuhusu viwango vipya ambapo Kenya ilipanda hadi nafasi ya 102.

•Mabingwa wa kombe la dunia Argentina wamesalia kileleni kwa pointi 1889.02, na Ufaransa wakichukua nambari mbili kwa pointi 1851.92.

Harambee Stars
Image: HISANI

Timu ya taifa ya soka ya Kenya imeonyesha kuimarika kidogo katika orodha ya hivi punde ya viwango vya kimataifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

Mnamo siku ya Alhamisi, Septemba 19, FIFA ilitoa ripoti kuhusu viwango vipya ambapo Kenya ilipanda hadi nafasi ya 102.

Harambee Stars hapo awali iliorodheshwa katika nafasi ya 108 duniani.

Katika orodha mpya, Kenya ina pointi 1208.96, kutoka pointi za awali ambazo zilikuwa 1197.73. Hiyo inaashiria kuboreshwa kwa pointi 11.23.

Maboresho hayo yanafuatia mafanikio ya hivi majuzi ya timu katika mechi za kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika 2025 dhidi ya Namibia na Zimbabwe.

Hivi majuzi, timu ya taifa ilipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Namibia na kutoka sare tasa dhidi ya Zimbabwe katika mchujo wa Kundi J uliochezwa mapema mwezi huu.

Stars kwa pamoja na Cameroon wanaongoza Kundi J  wakiwa na pointi nne lakini wana tofauti kubwa ya mabao na baadaye watacheza na mabingwa hao mara tano wa Afrika mnamo Oktoba 7 huku mechi ya marudiano ikipangwa Oktoba 15.

Morocco ndio taifa lililoorodheshwa katika nafasi ya kwanza barani Afrika huku ikiwa imeorodheshwa katika nafasi ya 14 duniani.

Mabingwa wa kombe la dunia Argentina wamesalia kileleni kwa pointi 1889.02, na Ufaransa wakichukua nambari mbili kwa pointi 1851.92.

Uhispania ipo katika nafasi ya tatu kwa pointi 1836.42, ikifuatiwa na England (4), Brazil (5) na Ubelgiji (6).

Mabingwa watetezi wa Afrika Ivory Coast wamepanda kwa nafasi tano kutoka nafasi ya 38 hadi 33 duniani na nafasi ya nne barani Afrika, huku mabingwa wa zamani Senegal wakipoteza nafasi mbili kutoka nafasi ya 19 hadi 21.

Kwa kulinganisha na mataifa jirani wa Afrika Mashariki, Uganda na Tanzania ziliorodheshwa katika nafasi za 90 na 110 mtawalia.

Wakati huo huo, Somalia, Burundi, Rwanda, na Sudan Kusini zimeorodheshwa katika nafasi ya 102, 136, 130, na 172.

View Comments