In Summary

•Arteta alifichua hayo wakati wa mkutano na waandishi wa habari Ijumaa kabla ya mechi ya The Blues dhidi ya Wanabunduki Jumamosi jioni.

•Arteta alisema Muargentina huyo, ambaye ni mkubwa kwake kwa miaka 10, alimwambia: "'Usijiingize katika ukocha. Ni ngumu sana'."

Mikel Arteta wa Arsenal
Image: GETTY IMAGES

Kocha wa Klabu ya Soka ya Arsenal, Mikel Arteta mnamo Ijumaa alifichua kwamba mwenzake wa Chelsea Mauricio Pochettino aliwahi kumshauri dhidi ya kujitosa katika ukufuzi.

Mhispania huyo mwenye umri wa miaka 41 alifichua hayo wakati wa mkutano na waandishi wa habari Ijumaa kabla ya mechi ya The Blues dhidi ya Wanabunduki Jumamosi jioni.

Arteta pia alimtambua kocha huyo wa zamani wa Tottenham Hotspurs ambaye alicheza naye katika klabu ya Paris-Saint Germain zaidi ya miongo miwili iliyopita kama mfano wake wa kuiga. Alizungumza mema kumhusu mkufunzi huyo mwenzake katika mkutano na waandishi wa habari kabla ya mechi ya Jumamosi.

"Ilikuwa nafasi yangu ya kwanza ya kitaaluma katika Paris na tulifika pamoja kwa wakati mmoja," Arteta alisema.

Mhispania huyo, ambaye wakati huo alikuwa kwa mkopo katika klabu PSG kutoka Barcelona aliongeza,"Tuliishi pamoja katika hoteli kwa miezi mitatu.

"Alikuwa mkosoaji. Amekuwa mmoja wa watu wenye ushawishi mkubwa katika taaluma yangu ya soka, kwanza kabisa kama mchezaji. Alinichukua kwenye mkono wake.

"Alinitunza kama mtoto mdogo, kama kaka mdogo, na alikuwa sehemu kubwa ya mafanikio niliyopata Paris kwa sababu alinitunza sana, alinipa ujasiri na ushauri mwingi.

“Amekuwa mfano kwangu tangu siku hiyo, si tu nilipokuwa mchezaji bali kama meneja pia kwa sababu nililazimika kufanya uamuzi wa kuacha kucheza na kuanza taaluma yangu ya ukocha.

"Alikuwa na mchango mkubwa katika hilo na nitaendelea kushukuru kwa kile amenifanyia."

Mchezaji huyo wa zamani wa kimataifa wa Uhispania alifichua kuwa Pochettino, ambaye amewahi kuwa mkufunzi wa Tottenham na PSG, alimwambia asiingie katika ukufunzi.

Arteta, akitabasamu, alisema Muargentina huyo, ambaye ni mkubwa kwake kwa miaka 10, alimwambia: "'Usijiingize katika ukocha. Ni ngumu sana'."

"Nilijua atakuwa kocha. Nilimfuata kwa karibu sana. Kama mchezaji tayari alikuwa kiongozi -- jinsi alivyokuwa anauelewa mchezo, alikuwa wa ajabu. Nilikuwa naye mgongoni mwangu na alikuwa mara kwa mara kunifundisha,” aliongeza.

Wachezaji wenza hao wa zamani ambao sasa ni makocha watakabiliana kama makocha kwenye uwanja wa Stamford Bridge siku ya Jumamosi, huku Arsenal wakipigania nafasi ya kwanza kwenye jedwali la Ligi ya Premia huku Chelsea wakisaka kuendeleza ufufuo wao wa hivi majuzi.

View Comments