In Summary

•Ronaldoalidai kuwa viongozi wa juu wa klabu hiyo wamekosa kumuamini katika nyakati ambapo amejaribu kuwaeleza kuhusu masaibu yake.

•Aliweka wazi kuwa, licha ya umahiri wake katika soka, kamwe hatawahi kuhatarisha afya ya familia yake juu ya mchezo huo.

Mshambulizi wa Manchester United Christiano Ronaldo. Amefichua kuwa hana raha katika klabu hiyo ya Premier league.
Image: GETTY IMAGES

Mshambulizi Christiano Ronaldo ameshtumu uongozi wa Manchester United kwa kumpuuza wakati anapokuwa akipitia mateso.

Katika mahojiano na Piers Morgan, mchezaji huyo wa kimataifa wa Ureno alidai kuwa viongozi wa juu wa klabu hiyo wamekosa kumuamini katika nyakati ambapo amejaribu kuwaeleza kuhusu masaibu yake.

Alitoa mfano wa wakati ambapo binti yake aliaga dunia siku chache tu baada ya kuzaliwa.

"Niliambia rais na mkurugenzi wa Manchester United lakini ni kama hawakuamini kuwa kuna kitu kibaya kilikuwa kikiendelea ambacho kilifanya nihisi vibaya," alisema.

Mshindi huyo wa Ballon d' Or mara tano alidai kwamba ingawa viongozi waliamini hali yake kwa mashaka, hawakuelewa kabisa kile alichokuwa akipitia.

Hata hivyo aliweka wazi kuwa, licha ya umahiri wake katika soka, kamwe hatawahi kuhatarisha afya ya familia yake juu ya mchezo huo.

"Sitawahi kuhatarisha afya ya familia kwa sababu ya soka, sio sasa ama miaka miaka kumi nyuma au mbele," alisema.

Aliongeza, "Ni jambo ambalo liliniumiza sana,  kuwa walitilia shaka maneno yangu kwamba niliteseka hasa wakati Bell na Geo walikaa wiki moja hospitalini kwa sababu Bell alikuwa na shida kubwa," 

Ronaldo aliweka wazi kwamba alishindwa kuandamana na kikosi cha Mashetani Wekundu kwenye maandalizi ya msimu kwa kuwa hangeweza kuacha familia yake wakati mwanawe akiwa amelazwa hospitalini.

Mshambuliaji huyo alidai kuwa uongozi wa klabu hiyo umekosa kumuelewa hata sasa ambapo binti yake ni mgonjwa.

Siku ya Jumatatu jioni, Manchester United hatimaye ilivunja ukimya kuhusu tetesi nzito za mshambulizi huyo wake.

Klabu hiyo ilisema inafahamu kuhusu mahojiano hayo na kutangaza itazingatia jibu lake baada ya ukweli wote kuthibitishwa.

"Lengo letu linasalia katika kujiandaa kwa kipindi cha pili cha msimu na kuendeleza kasi, imani na umoja unaojengwa miongoni mwa wachezaji, meneja, wafanyakazi na mashabiki," taarifa iliyotolewa Jumatatu jioni ilisoma.

View Comments