In Summary

•Grand P amesema kuwa kitendo cha kiungo huyo wa kati ni cha kujivunia na kinaonyesha ushujaa mkubwa.

•Rais wa Senegal Macky Sall ni miongoni mwa wale ambao wamejitokeza kusimama na mchezaji huyo wa zamani wa Everton.

Grand P, Idrissa Gueye
Image: HISANI

Mwanamuziki mashuhuri kutoka Guinea Moussa Sandiana Kaba ameonyesha kusimama na mchezaji wa PSG Idrissa Gueye kufuatia madai kuwa alisusia mechi ya Ligue 1 dhidi ya Montpellier kwa kuwa hakutaka kuvakia jezi yenye rangi za upinde wa mvua.

Grand P amesema kuwa kitendo cha kiungo huyo wa kati ni cha kujivunia na kinaonyesha ushujaa mkubwa.

"Hatujali. Idrissa Gueye, Afrika inajivunia wewe shujaa. Mungu akubariki," Grand P alisema kupitia Facebook

Rangi za upinde wa mvua kwa kawaida huwa ishara ya kuunga mkono jamii ya mashoga na wasagaji.

Wikendi iliyopita vilabu vya ligi ya Ufaransa vilikuwa vimeshawishiwa kuweka rangi za upinde wa mvua kwenye upande wa nyuma wa jezi za wachezaji wao ili kusherehekea Siku ya Dunia dhidi ya chuki ya wapenzi wa jinsia moja inayoadhimishwa Mei 17.

Vyombo vya habari nchini Ufaransa vimeripoti kuwa Gueye ambaye ni mfuasi sugu wa dini ya Kiislamu alisusia mechi hiyo kwa kuwa imani yake haimruhusu kuwa na uhusiano wowote na jamii hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kocha mkuu wa PSG Mauricio Pochettino alisema Gueye aliruhusiwa kutoshiriki mechi hiyo kwa "sababu za kibinafsi."

Hata hivyo ripoti nyingi zimeashiria kuwa raia huyo wa Senegal mwenye umri wa miaka 32 aligoma kushiriki mechi hiyo.

Huku kundi kubwa la watu na mashirikia wakipinga hatua ya Gueye, baadhi ya watu mashuhuri wakiwemo wachezaji na wasanii wakubwa haswa kutoka bara Afrika na ambao ni wafuasi wa dini ya Kiislamu wamejitokeza kumtetea mchezaji huyo.

Rais wa Senegal Macky Sall ni miongoni mwa wale ambao wamejitokeza kusimama na mchezaji huyo wa zamani wa Everton.

"Namuunga mkono Idrissa Gana Gueye. Misimamo yake ya kidini lazima iheshimiwe," Sall alisema kupitia Twitter.

Wachezaji wengine mashuhuri wakiwemo Cheikhou Kouyate wa Crystal Palace na Ismaila Sarr wa Watford pia wameonyesha kusimama na Gueye.

View Comments