In Summary

•Uhuru anasema mzozo wao ulitimbuka alipogundua mpango wa Ruto wa kumbandua kabla ya muhula wake kukamilika.

•Uhuru aliwaambia wazee hao kwamba alipounda serikali, Ruto alijaribu kufikia makubaliano ya mamlaka na kiongozi wa Chama cha ODM Raila Odinga.

Rais Uhuru Kenyatta
Image: MERCY MUMO

Rais Uhuru Kenyatta amesimulia jinsi naibu wake William Ruto alivyopanga kumng’oa mamlakani..

Kulingana na Standard, Uhuru anasema mzozo wao ulitimbuka alipogundua mpango wa Ruto wa kumbandua kabla ya muhula wake kukamilika.

Uhuru alisema hayo siku ya Jumamosi  alipokuwa anahutubia takriban viongozi  3000 kutoka eneo la Mlima Kenya.

Viongozi hao ni pamoja na wazee kutoka Kiama Kia Ma, Baraza la Wazee wa Kikuyu na viongozi waliochaguliwa.

Rais aliwaambia kwa nini Ruto hakuwafaa kama rais.

Kulingana na ripoti za Standard, Uhuru alisema alidanganywa kuchukua uongozi wa serikali huku Ruto akisimamia chama cha Jubilee.

Uhuru aliwaambia wazee hao kwamba alipounda serikali, Ruto alijaribu kufikia makubaliano ya mamlaka na kiongozi wa Chama cha ODM Raila Odinga.

"Rais alitufahamisha kuwa Ruto alikuwa akimfuata nyuma, akipanga jinsi atashirikiana na Raila ili kumbandua kwa wakati ufaao," Mbunge wa Mathioya Peter Kimari aliambia Standard.

Uhuru pia alidai kwamba Ruto alitaka Raila akamatwe na kufunguliwa mashtaka baada ya kuapishwa kama "rais wa watu" mnamo Januari 2018.

Wakati wa mkutano huo, pia ilifichuliwa kuwa Ruto alikuwa akihimiza maandamano ya upinzani mwaka wa 2017 huku akimchochea Uhuru kuyabana.

Mwezi uliopita, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju pia alidai Ruto hafai uongozi.

Tuju alidai kuwa naibu rais alipanga njama ya kuhujumu utawala wa Uhuru na kuifanya nchi isitawalike.

Ili kutekeleza mipango yake, Tuju alisema kuwa Ruto  alimwendea kiongozi wa ODM Raila Odinga muda mrefu kabla ya ‘Handshake’ mwakani 2018 ili kuunganisha nguvu na kushinda ajenda za Uhuru Bungeni.

"Alikuwa mtu wa kwanza kumwendea Raila ili wamtusi Rais," Tuju alisema.

Mnamo Januari, naibu mwenyekiti wa Jubilee David Murathe pia alidai kuwa Rais alikatisha mazungumzo yake na William Ruto kwa sababu alikuwa na nia ya kuhujumu utawala wake.

Murathe alisema Ruto alipewa nusu ya serikali zikiwemo baadhi ya wizara zenye nguvu lakini Rais hakuridhishwa na jinsi zilivyoendeshwa.

Mbunge huyo wa zamani alisema Uhuru aliamua kufanya kazi na Raila ili kuhakikisha kile alichotaka kuwafikishia Wakenya kinatimizwa.

Msemaji wa Ruto, Emmanuel Talam ambaye alizungumza na Star alihoji ni kwa nini madai haya yote hayakutolewa kabla ya uchaguzi wa 2017.

"Ruto alikuwa mtakatifu walipotaka kuchaguliwa tena lakini akawa mbaya punde tu! Wajinga waliisha Kenya," aliambia Star kwenye simu.

View Comments