In Summary

• Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano NCIC imetoa orodha ya misemo ya Kiswahili, Kiingereza na lugha nyingine za kienyeji ambayo inasema ni sawa na matamshi ya chuki.

• Maneno ya kashfa kama vile Madoadoa, Kama Mbaya Mbaya na Sipangwingwi yamekuwa misemo maarufu kwenye mikutano ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Mwenyekiti wa NCIC Kasisi Dkt. Samuel Kobia akiwa na bwana wa Slang Alessandro Olocho Santo almaarufu Madocho wakati wa mkutano na wanahabari wa NCIC Aprili 8,2022.
Image: The star/ Enos Teche

Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano NCIC imetoa orodha ya misemo ya Kiswahili, Kiingereza na lugha nyingine za kienyeji ambayo inasema ni sawa na matamshi ya chuki.

Tume hiyo inasema msemo maarufu 'sipangwingwi' ni miongoni mwa misemo ambayo ina matamshi ya kificho na ambayo inasawazishwa na matamshi ya chuki.

Nyingine ni Fumigation, Madoadoa, Mende, Kama Mbaya na Operation Linda Kura.

Mwenyekiti wa NCIC Samuel Kobia alisema maneno na miswemo hiyo sasa imepigwa marufuku katika mikutano ya hadhara, mitandao ya kijamii na vipindi vya mazungumzo ya kisiasa.

"Hii itasaidia pakubwa katika kudhibiti matamshi ya chuki na kuhakikisha taifa letu liko salama wakati huu wa kuandaa uchaguzi," alisema.

Mkakati huo unakuja baada ya dhoruba kutokana na matumizi ya neno 'madoadoa' katika mikutano ya hadhara.

Mtaalam wa misemo kama hiyo Alessandro Olocho Santo anayejulikana zaidi kama Madocho alikuwepo wakati wa mkutano wa wanahabari wa NCIC.

Maneno ya kashfa kama vile Madoadoa, Kama Mbaya Mbaya na Sipangwingwi yamekuwa misemo maarufu kwenye mikutano ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Matumizi ya msemo modoadoda (madoa) katika mikutano ya kisiasa katika siku za hivi majuzi umewaweka wanasiasa kadhaa matatani na tume hiyo. Miongoni mwao ni kinara wa ODM Raila Odinga na Seneta wa Meru Mithika Linturi.

Muungano wa Kenya Kwanza ukiongozwa na naibu rais William Ruto ndio wamekuwa katika mstari wa mbele kutumia msemo wa Sipangwingwi ambao unatokana na ngoma ya msanii Exrey aliyewashirikisha wasanii wenza Trio Mio na mwanadada wa kufoka Sylivia Ssaru.

View Comments