In Summary

• Seneta wa Kakamega Cleophas Malala amesema akichaguliwa kama gavana ataweka 'hot showers' kila boma ili watu waoge kama wamesimama.

Seneta wa Kakamega Cleophas Malala
Image: Screengrab:YouTube

Seneta wa Kakamega Cleophas Malala amesema pindi tu atakapochaguliwa kama gavana wa pili wa kaunti hiyo kumrithi Wycliffe Oparanya, basi atapatia suala la maji kipaumbele katika wakaazi wote wa kaunti hiyo pana ya Magharibi mwa Kenya.

Akizungumza katika runinga moja nchini wakati anaendelea kujipigia debe kama gavana mtarajiwa wa kakamega katika uchaguzi wa Agosti 9, Malala aliahidi kwamba anawaonea huruma kina mama wazee ambao wanateseka kutembea safari ndefu kutafuta maji.

Alisema pindi atakapoingia katika kiti hicho ataunganisha kila boma na maji na pia kuweka bafu za maji moto katika kila boma ili watu waoge wakiwa wamesimama, kinyume na sasa ambapo wengi wanaoga maji baridi tena nje nyuma ya nyumba wakiwa wameinama kwa kuogopa kuonekana na watu.

“Mimi kwa masuala ya kina mama, nimesema nitainua hadhi ya kina mama, nitainua heshima ya kina mama. Mambo ya kina mama kwenda mtoni, kubeba maji na mtungi kwa kichwa wakisomba maji eti ndio nyungu ijae, mimi nitahakikisha kwa majaaliwa ya mwenyezi Mungu nitaunganisha mifereji kwa kila boma ili watu waache kufuata maji mtoni,” alisema Malala.

Alitolea mfano kwamba watoto wasichana wanapitia mitihani migumu wakati wanatoka shuleni na kulazimika kuenda mtoni kutafuta maji, safari ambazo aghalabu huwaletea majaribu ya kubakwa au hata kutongozwa na hivyo kusababisha mimba za mapema zinazodidimiza ndoto zao za masomo.

“Tuko na wazee, kina mama ambao hata hawawezi kuinama kwa bafu kuoga, unapata wameweka beseni maji kwa bafu, mama mzee hawezi inama kwa sababu magoti yao yameisha. Hawezi oga kama ameinama. Mimi nitafanya kitu rahisi sana, kwa sababu kama maji yamefika kwa nyumba yako, nitaweka ‘hot showers’ nataka watu wangu waoge kama wamesimama kwa sababu kuoga kama umesimama si jambo gumu,” alijipigia debe Malala.

Seneta huyo anapania kuwa gavana ajaye kwa tiketi ya chama cha ANC kilichopo ndani ya muungano wa Kenya Kwanza unaoongozwa na naibu rais William Ruto. Wiki moja iliyopita, Dkt. Boni Khalwale alijitoa katika kinyang'anyiro hicho na kumpa mkono Malala.

View Comments