In Summary

•Njogu alibwagwa chini na mbunge wa sasa Charity Kathambi katika uchaguzi huo uliofanyika Alhamisi.

•Mtangazaji huyo aliendelea kumpongeza Kathambi na kumtakia mema katika uchaguzi wa mwezi Agosti.

Image: FACEBOOK// NJOGU WA NJOROGE

Mtangazaji wa zamani wa Media Max John Njogu Njoroge, na ambaye alikuwa anawania kiti cha ubunge cha Njoro amekubali kushindwa baada ya kupoteza tikiti ya UDA katika kura ya mchujo.

Njogu alibwagwa chini na mbunge wa sasa Charity Kathambi katika uchaguzi huo uliofanyika Alhamisi.

Njogu amesema kwamba anaheshimu uamuzi wa wakazi wa Njoro na kuweka wazi kuwa ameridhika na chaguo lao.

"Watu wangu wa Njoro, ninaheshimu uamuzi wenu. Kwa waliosimama nami, Mungu awabariki sana. Azma, maono na ndoto yetu kwa Njoro imepitwa na maono bora. Tumeridhika," Njogu alisema kupitia ukurasa wake wa Facebook.

Mtangazaji huyo aliendelea kumpongeza Kathambi na kumtakia mema katika uchaguzi wa mwezi Agosti.

"Kwa wale wote walionisaidia kifedha, walioniombea na kunitakia heri, Mungu wangu awakumbuke katika wakati wenu wa shida.Na awalipeni na kubariki maisha yenu. Tunaanguka mara nyingi. Lakini tunapata nguvu ya kuinuka kutoka ndani. Mungu awabariki ninyi nyote," Alisema.

Kathambi kwa upande wake ametoa shukran kwa wakazi wa Njoro kwa kumteua kumchagua kupeperusha bendera ya UDA katika kinyang'anyiro cha ubunge.

Pia amewapongeza wanasiasa wengine waliochaguliwa kuwania viti vingine mbalimbali kwa tikiti ya UDA.

Kwa wale ambao kwa bahati mbaya walipata kura chache kuliko washindi, jipe matumaini. Nyote mlikuwa na ndoto ya jamii nzuri kwa watu wetu," Alisema.

Matokeo ya shughuli ya Alhamisi yanaendelea kutangazwa katika maeneo mbalimbali ya nchi.

View Comments