In Summary

• Jumatatu polisi kaunti ya Migori waliwakamata vijana 12 waliokuwa wakisdafirisha silaha kutatiza shughuli za mchujo wa chama cha ODM.

Pingu
Image: Radio Jambo

Jumatatu polisi katika kaunti ya Migori waliwatia mbaroni vijana 12 waliopatikana wakisafirisha silaha kali za kivita kuelekea vituo mbali mbali ambapo mchujo wa chama cha ODM ulikuwa unafanyika.

Kulingana na taarifa za polisi katika kaunti hiyo, kumi na wawili hao walinaswa wakisafirisha silaha hizo kwa magari mawili aina ya Probox, magari ambayo nambari zao za usajili zilikuwa zimefutwa.

Baada ya kukamatwa, polisi walipata silaha aina ya panga tano zilizoshibishwa kwa makali kweli kweli pamoja na rungu mbili, kitabu kilichokuwa na kumbukumbu za mkutano wa mmoja wa wagombeaji wa nafasi ya kisiasa katika kaunti hiyo.

Washukiwa hao walisemekana walikuwa mbioni kuelekea eneo bunge la Suna Magharibi ambapo kinyang’anyiro cha tiketi ya ODM baina ya mbunge wa sasa Peter Masara na mbunge wa zamani ambaye anataka kurejea katika kiti hicho, Joseph Ndiege.

Kumi na wawili hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani Jumanne asubuhi ili kujibu mashtaka dhidi ya kupatikana na silaha hatari pamoja ya kuwa na njama ya kuhujumu uchaguzi wa kura za mchujo wa chama cha ODM.

View Comments