In Summary

•Gavana Alfred Mutua ametangaza kuwa chama chake kimehamia kwenye muungano unaoongozwa na naibu rais William Ruto wa Kenya Kwanza.

Gavana wa Machakos Alfred Mutua
Image: MAKTABA

Chama cha Maendeleo Chap Chap kimejiondoa kwenye muungano wa Azimio La Umoja unaoongozwa na Raila Odinga na rais Kenyatta.

Gavana Alfred Mutua ametangaza kuwa chama chake kimehamia kwenye muungano unaoongozwa na naibu rais William Ruto wa Kenya Kwanza.

Akihutubia waandishi wa habari Jumatatu, Mutua amesema alitia saini mkataba na muungano wa Kenya Kwanza jioni ya Jumapili.

"Naibu Rais William Ruto ni mtu mzuri na ataibadilisha nchi hii. Jana usiku (Jumapili) tulitia saini mkataba na Kenya Kwanza na nakala hii hapa," Mutua alisema.

Mnamo Ijumaa, Mutua alidai kuwa Msajili na Muungano wa Azimio La Umoja-One Kenya walikataa kuwapa nakala ya mkataba wa muungano wa Azimio.

Hapo awali kiongozi wa chama cha Ford Kenya Moses Wetang'ula alikuwa amewakaribisha Mutua na Amason Kingi wa PAA kwenye muungano wao.

Wetangula aliwapongeza wawili hao kwa hatua waliyopiga  na kusema itaongeza muungano huo nguvu tunapokaribia uchaguzi mkuu.

"Hongera vyama vya siasa vya Maendeleo Chap Chap na PAA kwa kujiunga na Muungano wa Muungano wa Kenya Kwanza. Nguvu yenu inaleta nguvu zaidi na inatuhakikishia  ushindi wa Kenya Kwanza Alliance katika uchaguzi Mkuu wa Agosti 9. Hongera," alisema.

Kingi hata hivyo bado hajatoa matamshi yake rasmi kuhusu suala hilo.

Mutua na Kingi wamekuwa wakilalamikia kutengwa katika muungano wa Azimio.

View Comments