In Summary

•Wazee hao wameshauri muungano wa Azimio na viongozi wake kuwa Karua ndiye anayefaa zaidi kwa nafasi hiyo kati ya wote wanayoimezea mate.

•Wazee hao walipongeza muungano wa Azimio la Umoja kwa kutumia njia ya jopo kuteua mgombea mwenza.

Raila Odinga na kiongozi wa Narc Martha Karua
Image: FACEBOOK// MARTHA KARUA

Makundi mawili ya wazee kutoka jamii ya Kikuyu, Baraza la wazee wa Kikuyu na Kiama kia Ma yamempendekeza kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua kuwa mgombea mwenza wa Raila Odinga.

Wakihutubia waandishi wa habari katika ofisi zao zilizo Ruaka, wazee hao walipongeza muungano wa Azimio la Umoja kwa kutumia njia ya jopo kuteua mgombea mwenza.

Wazee hao wamesema inagwa wanasimama na wanasiasa wote wanne kutoka Mlima Kenya ambao wamefika mbele ya jopo la Azimio, itakuwa furaha yao kuona Martha Karua akipatiwa wadhifa huo.

"Kutokana na uzoefu na mambo tunayofuatilia, tumekubaliana ni Martha Karua. Tumesema tutafurahi sana kama jamii ikiwa Martha Karua ndiye Azimio watachua kama mgombea mwenza na hatimaye kuwa naibu rais," Msemaji wa wazee hao Wachira wa Kiago alisema.

Wazee hao wameshauri muungano wa Azimio na viongozi wake kuwa Karua ndiye anayefaa zaidi kwa nafasi hiyo kati ya wote wanayoimezea mate.

Haya yanajiri huku jopo la kuteua mgombea mwenza wa Raila likiwa limesalia na masaa machache tu kukamilisha shughuli ya kuwahoji wanasiasa mbalimbali wanaotaka wadhifa huo.

Jumanne asubuhi kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka alifika mbele ya jopo hilo licha ya kutishia kutohudhuria mahojiano hayo hapo awali.

Kalonzo aliweka kando vitisho vyake vya awali kuwa hawezi kufika mbele ya jopo hilo na kuwasili katika Hoteli ya Serena mwendo wa saa tatu asubuhi.

Jopo la Azimio limewahoji wanasiasa wanne kutoka Mlima Kenya wakiwemo Martha Karua, Peter Kenneth, Sabina Chege na gavana Lee Kinyajui.

View Comments