In Summary

•Mkataba wa Spika Muturi na Muungano wa Kenya Kwanza umetangazwa kuwa batili katika Mahakama  ya Mizozo ya Vyama vya Kisiasa.

•Mahakama pia ilikubaliana na ombi la wanachama kuwa uteuzi wa Muturi kama kiongozi wa chama ni kinyume na maagizo ya katiba.

Spika Justin Muturi atia saini mkataba na DP William Ruto anapojiunga na Kenya Kwanza Jumamosi, Aprili 9, 2022.
Image: MAKTABA

Mkataba wa muungano wa Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi na Muungano wa Kenya Kwanza umetangazwa kuwa batili katika Mahakama  ya Mizozo ya Vyama vya Kisiasa.

Mahakama hiyo pia ilitoa uamuzi sawa kuhusu nafasi yake kama kiongozi wa chama cha DP.

Muturi alikuwa ametia saini mkataba wa muungano nachama cha Naibu Rais William Ruto cha UDA, ANC ya Musalia Mudavadi  na Ford Kenya cha Moses Wetangula, ambavyo ni wanachama waanzilishi wa muungano wa Kenya Kwanza, kwa niaba ya chama cha DP.

Mkataba huo ulimaanisha kuwa chama cha DP kimekuwa mmoja wa wanachama wa muungano wa Kenya Kwanza.

"...Mkataba wa muungano unaodaiwa kuwa uliingiwa na upande wa tatu unaohusika na mhusika wa kwanza kwa niaba ya chama cha Democratic Party of Kenya ulifanywa bila mamlaka ya Chama cha Democratic Party of Kenya na ni batili".

Ombi la kupinga nafasi yake kama kiongozi wa chama na kushughulikia Ruto liliwasilishwa na maafisa watatu wa chama cha DP; Wambugu Nyamu, Daniel Munene na King'ori Choto.

Watatu hao waliteta kuwa Muturi alichukua nafasi ya kiongozi wa DP kwa nguvu licha ya upinzani kutoka kwa wanachama wa chama.

Mahakama hiyo ilikubaliana na waliowasilisha maombi kuwa uteuzi wa Muturi kama kiongozi wa chama ni kinyume na maagizo ya katiba ya chama ambayo inaelekeza lazima mtu awe mwanachama kwa angalau mwaka mmoja.

"Uteuzi wa mhojiwa wa kwanza (Justin Muturi) kama kiongozi wa chama cha Democratic Party of Kenya na Kongamano Maalum la Wajumbe wa Kitaifa tarehe 2 Februari 2022, haukuwa wa kitaratibu na hivyo kutangazwa kuwa batili," mahakama hiyo iliamua.

Uamuzi huo ulitolewa na Jessica M'mbetsa, mwenyekiti, na Wajumbe Samuel Nderitu na Adelaide Mbithi.

View Comments