In Summary

• Chebukati alimtangaza Raila kama mgombeaji urais katika uchaguzi wa Agosti 9 Jumapili mwendo wa saa tano asubuhi.

•Akizungumza baada ya kupokea cheti cha uteuzi, Raila alieleza imani yake Raila kwa IEBC kufanya uchaguzi wa huru na wa haki.

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati akimkabidhi mgombea urais wa Azimio la Umoja cheti cha uteuzi mnamo Juni 5, 2022.
Image: IEBC

Mgombea urais wa muungano wa Azimio la Umoja- One Kenya Raila Odinga hatimaye ameidhinishwa kuwania kiti hicho.

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alimtangaza Raila kama mgombeaji urais katika uchaguzi wa Agosti 9 Jumapili mwendo wa saa tano asubuhi.

"Nimeidhinisha uteuzi wa Raila Odinga kama mgombeaji Urais Agosti 9, 2022," Chebukati alisema.

Raila aliwasili katika ukumbi wa Bomas of Kenya dakika kadhaa baada ya saa nne akiwa ameandamana na mgombea mwenza wake Martha Karua na viongozi wengine wanaomuunga mkono katika kinyang'anyiro cha mwaka huu.

Akizungumza baada ya kupokea cheti cha uteuzi, Raila alieleza imani yake Raila kwa IEBC kufanya uchaguzi wa huru na wa haki.

"Tunafurahia kuwa hapa na kutimiza matakwa yote ya tume. Tuna imani kuwa IEBC ina uwezo wa kufanya uchaguzi huru na wa haki. Tunawaomba kufanya jinsi Wakenya wanavyotarajia kutoka kwenu," Raila alisema.

Raila alikuwa ameandamana na wanasiasa wengine wakiwemo Kalonzo Musyoka (Wiper) Gideon Moi (Seneta wa Baringo) Charity Ngilu (Gavana Kitui) Junnet Mohamed (MP Suna Mashariki) Timothy Bosire (Mweka Hazina wa ODM) Edwin Sifuna (Katibu Mkuu ODM ) Sabina Chege (Mwakilishi wa wanawake wa Muranga) Gavana Prof. Anyang' Nyong'o (Kisumu) Jeremiah Kioni ( MP Ndaragwa) Raphael Wanjala (MP Budalangi) John Waluke (Mbunge Sirsia) Gavana Ann Kananu (Nairobi) Maina Kamanda (Mbunge wa kuteuliwa) Esther Passaris (Mwakilishi wa wanawake Nairobi) Gavana Nderitu Muriithi (Laikipia) Timothy Wanyonyi (Mbunge Westlands) Ledama ole Kina (Seneta Narok)

Waziri huyo mkuu wa zamani alihakikishia tume ya IEBC kuwa yeye, wafuasi wake na viongozi wa Azimio watafuata sheria katika kampeni zao.

Aidha aliwasihi wafuasi wake wasihusike katika kuharibu vifaa vya kampeni vya wapinzani wake katika uchaguzi wa Agosti.

'Tunaahidi kuwa tutajiendeleza vizuri na kisheria..Tunaomba wafuasi wetu wasiharibu mabango ya wapinzani wetu," Alisema.

Pia aliweka wazi kuwa hana shida yoyote na vyombo vya habari huku akisema kuwa vina uhuru wa kufanya kazi bila kuingiliwa.

View Comments