In Summary

•Wajackoyah alisema kuwa sumu ya nyoka ina thamani kubwa ambayo inaweza kuendesha uchumi wa nchi.

•Wajackoyah alisema baada ya utoaji wa sumu nyoka hao watasafirishwa nje ya nchi kama chakula kwa nchi zinazokula nyama yake.

GEORGE WAJACKOYAH
Image: EZEKIEL AMING'A

Mgombea Urais kwa tikiti ya Roots Party of Kenya George Wajackoyah sasa anasema ufugaji wa nyoka pia utakuwa mkakati wake wa kuongeza mapato ya serikali na kulipa madeni ya nchi kwa mataifa mengine.

Wajackoyah ambaye alivuma sana kutokana na ahadi yake ya kuhalalisha bangi, alisema ufugaji wa nyoka ni mradi wa faida ambao serikali yake itazingatia iwapo atachaguliwa katika uchaguzi wa Agosti 9.

Alifichua kuwa sumu ya nyoka ambayo inaweza kutolewa kutoka kwa nyoka wanaofugwa ina thamani kubwa ambayo inaweza kuendesha uchumi wa nchi sambamba na kilimo cha bangi.

"Tunaanzisha ufugaji wa nyoka nchini ili tuweze kukamua sumu ya nyoka kwa madhumuni ya dawa, watu wengi wanaumwa na nyoka hapa nchini na inabidi msubiri dozi kutoka nje ya nchi kupitia shirikisho la dawa," Wajackoya alisema katika mahojiano na Citizen TV Jumatano jioni.

Wajackoyah alisema baada ya utoaji wa sumu nyoka hao watasafirishwa nje ya nchi kama chakula kwa nchi zinazokula nyama yake.

Hii, alisema, itazalisha mapato ambayo yanaweza kulipa deni kubwa la nchi.

"Tuna walaji nyoka wengi kama Wachina. Moja ya njia tunazoweza kulipa madeni ya Wachina ni kutoa sumu kutoka kwa nyoka na kuwapa Wachina nyama ya kula na kuwaambia ni malipo ya deni."

Mgombea huyo wa urais ni mmoja wa wanne ambao IEBC ilipatia kibali cha kuwania kiti hicho cha juu zaidi kwenye uchaguzi wa Agosti 9, mwaka huu.

Wengine ni pamoja na kinara wa ODM Raila Odinga, Naibu Rais William Ruto na David Wahiga Mwaure wa Agano

Wajackoyah pia amevuma kwa kupendekeza hatua kali kama vile kutupilia mbali katiba ya Kenya na kutawala kwa sheria zake iwapo atachaguliwa.

Hatua hizo, anasema, zitamwezesha kugeuza hali ya uchumi wa nchi na kutokomeza ufisadi.

View Comments