In Summary

•Ruto aliwakashifu wapinzani wake kwa kueneza propaganda kwamba Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja ameghushi stakabadhi za masomo.

•Aliwashutumu Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga kwa kupanga kubadilisha katiba na kubuni nyadhifa nyingi zaidi iwapo watashinda uchaguzi huo.

DP William Ruto
Image: DPPS

Naibu Rais William Ruto ameagiza ‘deep state’ kukoma kuwatisha wafuasi wake na badala yake wakabiliane naye moja kwa moja.

Akiongea katika uwanja wa Mayuba wakati wa mkutano wa Kenya Kwanza mnamo Ijumaa, Ruto aliwakashifu wapinzani wake kwa kueneza propaganda kwamba Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja ameghushi stakabadhi za masomo.

Hata hivyo, Ruto alisema kuwa Raila Odinga hatamshinda katika uchaguzi wa Agosti, akiongeza kuwa ‘deep state’ imepanga mikakati ambapo wamewaamuru maafisa wa Ikulu kuzuia azma yake (Ruto).

"Sijui kwa nini timu ya Azimio ina wasiwasi sana kuhusu uchaguzi wa Agosti. Nataka kuwaambia kuwa timu yangu imejiandaa kwa ajili yao,” alisema.

DP alisema serikali yake ya Kenya Kwanza itajumuisha watu wote serikalini ili kuhakikisha kila Mkenya ananufaika.

Aliwashutumu Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga kwa kupanga kubadilisha katiba na kubuni nyadhifa nyingi zaidi iwapo watashinda uchaguzi huo.

“Ikiwa unataka kufurahia uchumi wa nchi hii basi upige kura kwa busara katika uchaguzi wa Agosti. Msiwapigie kura watu ambao hawana itikadi ya ugatuzi," Ruto alisema.

Mgombea urais wa Kenya Kwanza alisema amefanya mengi katika eneo la Magharibi katika miaka yake tisa katika siasa.

Alitoa mfano wa Bungoma ambapo alisema aliweza kufadhili ujenzi wa barabara ya lami ya Chwele-Lwakhakha, Taasisi ya Sirisia Technical Training Institute na kuwaunganishia wananchi umeme

“Sitembei hapa Sirisia kwa mara ya kwanza. Nilifanya kazi na mbunge wenu John Waluke kabla ya kuombwa aende kupiga magoti na kuabudu baadhi ya watu wachache ili aruhusiwe kushiriki,” Ruto alisema.

DP alisema ikiwa atajinyakulia mamlaka, serikali yake ya Kenya Kwanza itatenga Sh100 bilioni ambazo zitasaidia vijana katika kubuni nafasi za kazi.

"Lengo kuu la kuungana na mkuu wa Ford Kenya Moses Wetang'ula na kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi ni kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wote wadogo wananufaika," alisema.

Kwa upande wake, Seneta wa Bungoma Wetang’ula alisema kuwa pande zote mbili chini ya mwavuli wa Kenya Kwanza zina makubaliano halali ya kufanya kazi ambayo yatawawezesha Wakenya kufaidika.

Kiongozi huyo wa Ford Kenya alihimiza eneo hilo kukataa ombi la Raila, akisema kuwa wamekuwa likimuunga mkono kwa miaka mingi.

Alisema iwapo Kenya Kwanza itanyakua uongozi, chakula na pembejeo za kilimo zitapunguzwa ili kuweza kumudu kila Mkenya.

Mgombea wa kiti cha ugavana kaunti ya Bungoma Ken Lusaka alisema kuwa atasitisha vikao vyake wiki ijayo Jumanne ili kujitokeza na kuangazia kampeni za Kenya Kwanza.

Lusaka alisema yuko tayari kukabiliana na mpinzani wake wa kisiasa Gavana Wycliffe Wangamati.

View Comments