In Summary

•DP  alisema hatawaruhusu Wachina wajishughulishe na biashara kama vile kuchoma mahindi, kuuza kwenye vibanda, miongoni mwa zingine. 

•DP alibainisha kuwa Kenya ina makubaliano na mataifa mengine kuhusu kiwango cha biashara na kazi zinazoweza kufanywa na wageni na wenyeji. 

DP William Ruto
Image: DPPS

Naibu Rais William Ruto amesema kuwa atawafukuza raia wa Uchina wanaojihusisha na biashara za rejareja zinazoweza kufanywa na wakenya.

Kulingana na gazeti la Daily Nation, DP  alisema iwapo atachaguliwa kuwa rais mnamo Agosti 9, hatawaruhusu Wachina wajishughulishe na biashara kama vile kuchoma mahindi, kuuza kwenye vibanda, miongoni mwa zingine. 

Akizungumza wakati wa Kongamano la Kiuchumi la Kenya Kwanza jijini Nairobi, alisema hili halitafanyika, hata hivyo Wakenya wengi wanahangaika na ukosefu wa ajira. 

"Hizi ni biashara za Kenya na kwa wale wanaojishughulisha nazo, tuna ndege za kutosha kuwarudisha walikotoka," Ruto alisema. 

DP alibainisha kuwa Kenya ina makubaliano na mataifa mengine kuhusu kiwango cha biashara na kazi ambazo zinaweza kufanywa na wageni na wenyeji. 

Ruto aliongeza kuwa mikataba hiyo pia inabainisha mahali ambapo vibali vya kufanya kazi vinahitajika na mahali ambapo havihitajiki.

 "Kiwango hicho hakiuzwi kwenye vibanda, rejareja au mahindi ya kuchoma," alisema. 

Matamshi ya Ruto yalifuatia wasiwasi wa mfanyibiashara mmoja aliyekuwepo kwenye kongamano hilo aliyesema kuwa Wachina hao walivamia soko la reja reja na walikuwa wakiuza bidhaa kwa bei nafuu, jambo ambalo linatishia kuwepo kwao kama wafanyabiashara wa humu nchini. 

Matamshi ya DP pia yalikaririwa na Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria ambaye alisisitiza kwamba lazima Wachina wazuiwe  kufanya hivyo, "kwa sababu huwezi kupata mchuuzi nchini mwao." 

Kuria aliongeza kuwa Wachina lazima pia wakumbushwe kuwa deni ambalo Kenya inadaiwa itabidi lijadiliwe upya. 

"Naunga mkono suala hili la Wachina na ndege zikijaa tunaweza kuziweka kwenye mikokoteni. Je, kuna mfanyabiashara Mwafrika huko Beijing? Na nataka kuwawekea taarifa kwamba hatutawapeleka tu bali deni tunalodaiwa. ni lazima tukae na kujadili na kupanga upya na kupanga upya,” alisema.

View Comments