Mgombeaji wa urais wa chama cha Roots George Wajakoya akiwasili katika eneo la BOMAS of Kenya kuwasilisha stakabadhi za kuania urais kwa IEBC/EZEKIEL AMING'A

Mgombea urais wa chama cha Roots Party of Kenya George Wajackoyah sasa anasema wanawake wajawazito watapewa marupurupu kuanzia watakapopata mimba iwapo atashinda urais katika uchaguzi wa Agosti 9.

Akizungumza wakati wa mahojiano kwenye runinga moja hapa nchini, Wajackoyah alisema wanawake wajawazito watachukuliwa kuwa mali ya serikali mara tu watakapothibitishwa kisayansi kuwa wajawazito.

"Tunataka kumtunza mama kutoka  wakati wa uja uzito hadi anapojifungua, hii ni kwa sababu tutakuwa na pesa za kutosha kutoka kwa  bangi kuwatunza wanawake wetu," alisema.

Wajackoyah aliendelea kusema kuwa serikali yake itawapa likizo wanawake kuanzia wanapokuwa na ujauzito  hadi mtoto atakapozaliwa.

"Nitashirikiana na wataalamu kubaini ni muda gani mwanamke anahitaji kupumzika baada ya kupata ujauzito na kujifungua. Nitashauriana na Wakanada ambao wamepata haki katika kutunza wanawake," alisema.

Wajackoyah amekuwa maarufu kufuatia ahadi yake ya kuhalalisha bangi iwapo atachaguliwa mwezi Agosti.

Anasisitiza bangi ndio suluhu la kufufua uchumi wa Kenya unaodorora na kulipia deni la umma ambayo sasa imechangia maisha mangumu hapa nchini.

Mgombea huyo anatajwa kuwa farasi wa tatu katika kinyang'anyiro hicho kinachotarajiwa kufanyika Agosti 9, 2022, huku wadadisi wakisema huenda akalazimisha mchujo wa pili.

Washindani wengine katika kinyang'anyiro hicho ni naibu rais William Ruto ambaye atatumia bendera ya Kenya kwanza kuwania kiti hicho, pamoja na mgombea wa Urais  wa Azimio one Kenya Raila Amollo odinga.


View Comments